Kuendelea kutokota mvukuto wa kisiasa nchini Gambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21304-kuendelea_kutokota_mvukuto_wa_kisiasa_nchini_gambia
Askari wa vikosi vya usalama nchini Gambia wamesambazwa kwenye maeneo ya mji mkuu Banjul kufuatia hatua ya Rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh kukataa matokeo yanayoonesha kuwa alishindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe mosi ya mwezi huu wa Desemba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 12, 2016 23:16 UTC
  • Kuendelea kutokota mvukuto wa kisiasa nchini Gambia

Askari wa vikosi vya usalama nchini Gambia wamesambazwa kwenye maeneo ya mji mkuu Banjul kufuatia hatua ya Rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh kukataa matokeo yanayoonesha kuwa alishindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe mosi ya mwezi huu wa Desemba.

Wiki iliyopita, Jammeh aliwashangaza na kuwaacha vinywa wazi Wagambia na duru za kisiasa barani Afrika alipoyakataa katakata matokeo ya uchaguzi, kama alivyopongezwa na kila mtu alipojitokeza hadharani siku ya tarehe Pili Desemba kumpongeza Adama Barrow, mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa vyama vya upinzani hata kabla hajatangazwa mshindi rasmi wa kinyang'anyiro hicho.

Rais Jammeh aliyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais kwa madai ya kile alichokiita makosa yasiyokubalika yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Gambia na kutaka uitishwe uchaguzi mwingine mpya. Baada ya kura kuhesabiwa tena, yalitokea mabadiliko ya idadi ya kura zipatazo 19,000, lakini pamoja na hayo Adama Barrow alitangazwa mshindi wa uchaguzi kwa kujipatia asilimia 43.29 ya kura kulinganisha na asilimia 39.64 alizopata Yahya Jammeh. Hata hivyo inaonekana Jammeh amedhamiria kuwasilisha malalamiko ya kisheria kwenye Mahakama Kuu ya Gambia kupinga matokeo ya uchaguzi wa tarehe mosi Desemba.

Adama Barrow, mshindi wa uchaguzi wa rais Gambia

Wadadisi wa mambo wanasema, Jammeh ameamua kusambaza askari polisi na wa vikosi vya usalama katika barabara za mji wa Banjul kabla ya kufikisha malalamiko yake Mahakama Kuu ili kuweza kuwa na udhibiti kamili wa nchi. Rais huyo wa Gambia ametoa onyo kwa wananchi na kwa wafuasi wa Barrow kwamba wasijaribu kuonesha upinzani kwa kuingia barabarani na kutaka kuzipa tena taasisi za haki za kutetea za binadamu fursa ya kuiandama kwa shutuma na lawama kali serikali ya nchi hiyo. Matamshi hayo yanaonyesha kuwa uamuzi wa rais wa Gambia wa kuyakataa matokeo ya uchaguzi na kutoa onyo la kutumia mkono wa chuma kuyakandamiza maandamano ya wananchi vitavuruga uthabiti na kuzidisha mivutano ya kisiasa nchini humo.

Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na mwenyekiti wa ECOWAS

Jammeh ameonesha kuwa na azma thabiti ya kuendelea kubaki madarakani kufikia hadi ya kuizuia ndege iliyombeba Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia isitue katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Banjul. Sirleaf, ambaye ni mwenyekiti wa mzunguko wa Jumuiya ya Uchumi ya Magharbi mwa Afrika (ECOWAS), alitumwa na jumuiya hiyo kwenda nchini Gambia kufuatilia mgogoro huo wa uchaguzi uliojitokeza. Kutokana na msimamo wa Jammeh wa kuyakataa matokeo ya uchaguzi, kiongozi huyo sasa anaandamwa na wimbi la lawama za jamii ya kimataifa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limemtaka rais huyo wa Gambia aheshimu matakwa ya wananchi kwa kuyakubali matokeo ya uchaguzi bila ya masharti yoyote na kukabidhi madaraka kwa rais aliyechaguliwa.

Wafuasi wa Adama Barrow wakisherehekea ushindi wake

Uamuzi wa kukataa matokeo ya uchaguzi, katika kipindi hiki ambapo kila mtu alikuwa anatarajia kwamba baada ya miaka 22 ya utawala wa Yahya Jammeh, kwa mara ya kwanza Gambia itashuhudia makabidhiano ya amani ya madaraka, ni hatua hatari inayotishia amani ya nchi na usalama wa wananchi. Ung'ang'anizi wa Rais Jammeh wa kubakia madarakani unafanana na kile kilichotokea takribani miaka saba nyuma wakati aliyekuwa Rais wa Ivory Coast wakati huo Laurent Gbagbo alipoyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyoonesha kuwa ameshindwa na kuitumbukiza nchi hiyo kwenye lindi la machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Matokeo ya mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiuchumi uliozuka nchini Ivory Coast yalikuwa ni kuifungulia njia Ufaransa ya kujiingiza kijeshi nchini humo. Ni hofu ya kujirudia tena hali hiyo ndiyo iliyomfanya Rais wa Liberia na mwenyekiti wa ECOWAS afanye safari ya haraka kuelekea Banjul. Viongozi wa nchi jirani na Gambia katika eneo la magharibi mwa Afrika wana wasiwasi wa kuvurugika amani na kujitokeza hali ya mchafukoge nchini humo; na ndiyo maana wanataka matakwa ya wananchi yaheshimiwe; na rais mteule Adama Barrow akabidhiwe hatamu za uongozi kwa njia ya amani…/