Amnesty yaijia juu Algeria kwa kuwatimua wakimbizi wa Mali
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Algeria kuunda sheria itakayowapa wakimbizi haki ya kupewa hifadhi sambamba na kuchunguza hatua ya kufukuzwa nchini humo wakimbizi wa Mali mapema mwezi huu.
Taarifa iliyotolewa jana (Jumapili) na Amnesty International tawi la Algeria imekosoa sheria ya nchi hiyo inayopiga marufuku wahamiaji haramu kupewa hifadhi na kuwahukumu vifungo jela wale wanaowasaidia wahamiaji hao kuingia nchini humo.
Amnesty International imeitaka serikali Algeria kuanzisha uchunguzi huru kuhusu hatua ya kufukuzwa nchini humo mamia ya wakimbizi kutoka Mali na vile vile wahamiaji wengine kutoka eneo la chini za jangwa la Sahara.
Siku ya Jumamosi serikali ya Algeria ilikanusha madai kuwa iliwatimua wakimbizi 260 raia wa Mali mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba. Iliarifiwa kuwa, mamia ya wakimbizi hao wa Kiafrika waliofukuzwa nchini Algeria waliingia katika nchi jirani ya Niger.
Vyombo vya habari viliripoti habari hiyo na kuwanukuu mashuhuda wakisema kuwa, wakimbizi hao kutoka nchi za Niger, Mali, Guinea na Senegal wameingia nchini Niger kwa kutumia malori matano ya Algeria yaliongozwa na vikosi vya usalama vya Niger.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2014 pia, wakimbizi elfu tatu wa Niger walirejeshwa nchini kwao kutoka Algeria. Vile vile mwezi Oktoba 2013, raia 92 wa Niger wakiwemo watoto wadogo 52 na wanawake 33 wakazi wa eneo la Zinder la kusini mwa Niger walipoteza maisha katika mpaka wa nchi hiyo na Algeria baada ya maafisa wa Algeria kuwapiga marufuku kuingia kwenye ardhi ya nchi hiyo.