Burundi yatishia kuondoa wanajeshi wake Somalia
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ametishia kuwa atawaondoa wanajeshi wa nchi yake walioko Somalia iwapo askari hao wanaohudumu katika kikosi cha Umoja wa Afrika UNISOM hawatalipwa mshahara wao.
Rais wa Burundi ameeleza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo ambao ni sehemu ya kikosi cha kudumisha amani cha Umoja wa Afrika hawakwenda Somalia kwa ajili ya kupata mapato, bali walitumwa huko kuisadia nchi hiyo. Burundi ni nchi yenye wanajeshi wengi zaidi katika kikosi cha kudumisha amani cha Umoja wa Afrika huko Somalia baada ya Uganda ambayo ina wanajeshi 5400. Kikosi cha kudumisha amani cha Umoja wa Afrika kilichoko Somalia kina jumla ya wanajeshi elfu 22. Kikosi hicho kimetumwa Somalia lengo likiwa ni kuendesha mapambano ya kulitokomeza kundi la kigaidi la wanamgambo wa al Shabab ambalo linataka kuipindua serikali kuu ya Somalia. Umoja wa Ulaya ndio unaowalipa wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika huko Somalia.
Hii ni katika hali ambayo miezi kadhaa imepita sasa ambapo Umoja wa Ulaya haujakabidhi pesa kwa viongozi wa serikali ya Bujumbura. Kwa mujibu wa mpango uliopita, ilitazamiwa kuwa Umoja wa Ulaya ingekuwa taasisi ya kwanza fadhili kwa Burundi kuipatia nchi hiyo kiasai cha yuro milioni 430 kati ya mwaka 2015 hadi 2020. Umoja wa Ulaya hivi sasa umesimamisha kuisaidia Burundi kiasi hicho cha fedha ili kuizuia serikali ya Bujumbura kutumia fedha hizo katika shughuli nyinginezo. Hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya imepelekea kuongezeka mivutano kati yake na Burundi.
Burundi inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa kwa muda sasa tokea kufanyika uchaguzi wa rais, ambapo Pierre Nkurunziza aliibuka mshindi. Hata kama kidhahiri hali ya Burundi inaonekana kuwa ya utulivu, lakini ripoti mbalimbali zinaashiria kupamba moto hali ya wasiwasi nchini humo. Siku kadhaa zilizopita wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa walibainisha wasiwasi wao kuhusu vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wapinzani huko Burundi. Kwa upande wao viongozi wa Burundi wamepinga ripoti zote hizo na kupunguza uhusiano wao na taasisi mbalimbali za kimataifa au kuukata kabisa. Hata kama hadi sasa kumefanyika mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo, lakini mazungumzo hayajazaa matunda. Pamoja na hayo yote, viongozi wa kimataifa na kieneo wangali wanaendeleza jitihada zao za kuanzisha tena mazungumzo, huku taasisi za kimataifa pia zikiiwekea Burundi mashinikizo mbalimbali vikiwemo vikwazo. Mivutano hiyo inajiri katika hali ambayo kuweko vikosi vya Burundi katika kikosi cha kudumisha amani cha Umoja wa Afrika huko Somalia na kuendesha vita dhidi ya kundi la kigaidi la al Shabab kumekuwa na athari nzuru na kunapasa kuzingatiwa.
Kwa msingi huo kuongezeka mashinikizo ya Umoja wa Ulaya kunaweza kuathiri mchakato wa kurejesha amani na uthabiti katika eneo. Oparesheni za kudumisha amani za kikosi cha AU nchini Somalia si tu kuwa zitaathirika vibaya iwapo viongozi wa Burundi watatekeleza kivitendo tishio lao hilo dhidi ya Umoja wa Ulaya, bali mchafuko yatashtadi katika eneo. Wakuu wa Umoja wa Ulaya hata hivyo wanaendelea kushikilia msimamo na uamuzi wao kuhusu hali ya Burundi; uamuzi ambao haijulikani ni kwa kiasi gani utasaidia kutatua kadhia ya nchi hiyo.