Rais wa Gambia aituhumu ECOWAS kuwa imemtangazia vita
Rais Yahya Jammeh wa Gambia ameishutumu Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS kuwa imemtangazia vita baada ya kutangaza kuwa inaviweka vikosi vyake ya jeshi katika hali ya tahadhari endapo kiongozi huyo atakataa kuondoka madarakani baada ya muhula wake wa uongozi kumalizika mnamo mwezi huu.
Katika hotuba ya mwaka mpya aliyotoa kupitia televisheni ya taifa, Jammeh, ambaye ameapa kubakia madarakani licha ya kushindwa na mpinzani wake Adama Barrow katika uchaguzi wa rais wa Desemba mosi, ameahidi pia kuilinda Gambia na uvamizi wowote kutoka nje.

Wiki iliyopita, Marcel de Souza, Rais wa Kamisheni ya ECOWAS alitangaza kuwa vikosi vya kijeshi vya jumuiya hiyo vimewekwa katika hali ya tahadhari.
Rais wa Gambia ambaye kipindi chake cha kuweko madarakani kinamalizika tarehe 19 ya mwezi huu wa Januari, awali alikuwa amekubali kushindwa, lakini akabadili mawazo siku kadhaa baadaye na kuyakataa matokeo ya uchaguzi, hivyo kuzusha hofu ya uwezekano wa mataifa ya eneo la magharibi mwa Afrika kuingilia kati na kumuondoa madarakani kwa nguvu.
Katika hotuba yake hiyo ya mwaka mpya Rais wa Gambia amesema, azimio lililopitishwa na ECOWAS kwamba itatumia kila njia iwezekanayo kuhakikisha matokeo ya ucahguzi wa rais wa Gambia yanaheshimiwa, ni kutangaza vita na kuivunjia heshima katiba ya nchi hiyo.
"Acha niweke wazi kabisa, kwamba tuko tayari kuilinda nchi yetu dhidi ya uvamizi wowote ule….serikali yangu katu haitopendelea makabiliano kama hayo, lakini kulinda mamlaka yetu ya kujitawala ni jukumu takatifu kwa wazalendo wote wa Gambia", amesema kiongozi huyo.

Mpatanishi wa ECOWAS, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amempa Jammeh pendekezo la "kuondoka kwa heshima", lakini kiongozi huyo wa Gambia amelikataa kwa kudai jumuiya hiyo ya uchumi ya Afrika Magharibi imepoteza sifa ya upatanishi kwa kuwa msimamo wake si wa kutopendelea upande wowote…/