UN yataka kuungwa mkono juhudi za kukabidhiana madaraka kwa amani nchini Gambia
Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa magharibi mwa Afrika ameitaka jamii ya kimataifa kusaidia juhudi za kukabidhiwa madaraka kwa njia ya amani nchini Gambia.
Shirika la Habari la IRIB limemnukuu Mohamed Ibn Chambas, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa magharibi mwa Afrika ambaye ni raia wa Ghana akisema katika ripoti yake kwa Baraza la Usalama la umoja huo kuhusiana na Gambia kuwa, hivi sasa Umoja wa Mataifa unashirikiana na serikali ya Gambia lakini kuna ulazima kwa jamii ya kimataifa nayo kusaidia juhudi za kuhakikisha madaraka yanakambidhiwa kwa njia amani nchini humo.

Ameongeza kuwa, Umoja wa Mataifa ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS zinafanya juhudi za kuleta umoja wa kitaifa na kukabidhiwa madaraka kwa njia za usalama na amani nchini Gambia.
Itakumbukwa kuwa baada ya kuitawala kwa mkono wa chuma nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika kwa muda wa miaka 22, hatimaye Yahya Jammeh, rais wa zamani wa Gambia alilazimika kukimbia nchini humo tarehe 21 Januari mwaka huu baada ya nchi za magharibi mwa Afrika kutishia kutuma jeshi la kumuondoa kwa nguvu madarakani.

Jammeh alishindwa katika uchaguzi na Rais Adama Barrow wa hivi sasa wa nchi hiyo. Hata hivyo alikataa matokeo hayo na kudai kumefanyika udanganyifu, suala ambalo liliitumbukiza Gambia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiusalama.