UN yasisitiza kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Libya mwaka huu
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa, mwaka huu wa 2017 unapaswa kuwa mwaka wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya na kurejesha amani nchini humo.
Martin Kobler amesema kuwa mwaka huu wa 2017 unapasa kuwa mwaka wa kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro wa Libya ili nchi hiyo irejee katika hali ya amani na utulivu. Mjumbe huyo Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Abdulqadir Masahil Waziri Mshauri wa Algeria katika masuala ya Eneo la Maghreb, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Kobler ametilia mkazo pia udharura wa kurejeshwa amani na utulivu huko Libya.
Libya ilikumbwa na machafuko ya kisiasa tangu wakati wa kampeni ya mapinduzi ya wananchi mwaka 2011 yaliyoung'oa madarakani uongozi wa Kanali Muammar Gaddafi kwa uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za kieneo.
Kulindwa umoja wa ardhi, kuendelezwa mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi, kukabiliana na magenge ya magendo ya binadamu na wimbi la wahamiaji haramu kutoka nchi nyingine za Kiafrika kwa ajili ya kuelekea barani Ulaya, suala la kupungua uzalishaji wa mafuta na bei yake katika masoko ya kimataifa, ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili Libya hivi sasa.