Angola yaripoti kesi mbili za kwanza za ugonjwa wa Zika
Angola jana ilitangaza kuwa imesajili kesi mbili za awali za kirusi cha Zika, ikiwa imepita miezi mitatu baada ya kudhibitiwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya manjano ambao umeuwa nchini humo watu wasiopungua 400.
Zika ambao ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyobebwa na mbu umeenea katika nchi zaidi ya 60 tangu mlipuko wake kugunduliwa nchini Brazil mwaka juzi, na hivyo kuzidisha hofu kuhusu ugonjwa huo kuwa na uwezo wa kusababisha ulemavu kwa watoto wanaozaliwa. Jose Luis Gomes Sambo Waziri wa Afya wa Angola amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa nchi hiyo Luanda kwamba, hadi kufikia miezi miwili iliyopita Angola haikuwa na kesi yoyote ya ugonjwa wa Zika, lakini sasa tayari wameshasajili kesi mbili za Zika nchini humo.
Waziri wa Afya wa Angola ameongeza kuwa hatua za uzuiaji zinapaswa kuchukuliwa khususan zile za kuwaangamiza mbu wanaosambaza virusi hivyo. Ni muda mfupi umepita tangu Angola ikumbwe na mlipuko wa homa ya manjano ambayo ilianzia katika mji mkuu Luanda kabla ya kuenea kusini magharibi mwa nchi na kuingia hadi katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.