Jamii ya Asia inayoishi Kenya yataka kutambuliwa kama kabila la 44
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23389-jamii_ya_asia_inayoishi_kenya_yataka_kutambuliwa_kama_kabila_la_44
Wakenya wenye asili ya Asia wameitaka serikali ya Kenya iwatambue kama kabila la 44 na kuwapa haki zao za msingi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 13, 2017 04:15 UTC
  • Jamii ya Asia inayoishi Kenya yataka kutambuliwa kama kabila la 44

Wakenya wenye asili ya Asia wameitaka serikali ya Kenya iwatambue kama kabila la 44 na kuwapa haki zao za msingi.

Farah Mannzoor, Mkurugenzi Mkuu wa wakfu wa Mother’s Lap ameliambia gazeti la Nation linalochapishwa nchini Kenya kuwa, wakati umefika kwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuwatambua rasmi kama kabila la 44 kwa kuwa wametekeleza wajibu kama wazalendo sambamba na kutimiza masharti yote ya uraia, hivyo kuna haja watambuliwe rasmi.

Amesema jamii ya Asia iliwasili nchini humo mwaka 1820 kama wafanyabiashra na wajenzi na miaka ya 1890 wakishiriki katika mradi muhimu wa ujenzi wa reli inayoiunganisha nchi hiyo na Uganda. Amesema Waasia wana nafasi muhimu katika uchumi wa taifa, kutokana na namna walivyozagaa katika sekta mbalimbali na hususan biashara.  

Jamii ya Wamakonde walipoitembele Ikulu ya Rais, Nairobi, Oktoba 2016

Mwezi Oktoba mwaka jana, Kenya iliitambua rasmi jamii ya Wamakonde kama kabila la 43 mbali na Rais Uhuru Kenyatta kuiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kuharakisha mchakato wa kuwapa watu wa jamii hiyo vitambulisho vya kitaifa na hatimiliki za ardhi.

Agizo hilo lilitolewa baada ya watu wa jamii hiyo na ile ya Wapemba kufanya maandamano ya amani kutoka kaunti ya Kwale hadi Nairobi, wakiitaka serikali kuwatambua na kuwapa haki zao za kimsingi. Wamakonde ambao asili yao ni Msumbiji wamekuwa nchini Kenya tangu mwaka 1940.