Mali yamtaka Jammeh akabidhi madaraka kwa amani
-
Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa Mali
Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa Mali amemtaka Rais Yahya Jammeh wa Gambia akabidhi madaraka kwa amani na azuie nchi yake kutumbukia kwenye machafuko.
Rais wa Mali amesema, jambo la busara zaidi linalopaswa kufanywa na Yahya Jammeh ni kumkabidhi madaraka kwa amani rais aliyechaguliwa na wananchi, ifikapo tarehe 19 mwezi huu wa Januari.
Ikumbukwe kuwa mgogoro wa kisiasa wa Gambia ndio uliokuwa ajenda kuu katika kikao cha pamoja cha Mali na Ufaransa kilichofanyika Bamako, mji mkuu wa Mali.
Wakati huo huo nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS zimelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutuma wanajeshi nchini Gambia ili kumlazimisha Yahya Jammeh akabidhi madaraka kwa rais aliyechaguliwa na wananchi.
Kabla ya hapo ECOWAS ilikuwa imetangaza kuwa, kama juhudi za kidiplomasia za kumshawishi Yahya Jammeh akabidhi madaraka zitashindwa, itakuwa ni jukumu la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kumuondoa madarakani kwa nguvu Yahya Jammeh ambaye ameitawala Gambia kwa miaka 22 sasa.
Yahya Jammeh alishindwa kwenye uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe Mosi mwezi uliopita wa Disemba na awali alikubali kushindwa, lakini baadaye alibadilisha msimamo na kudai kuwa kumefanyika udanganyifu katika kuhesabu kura.
Mgombea wa upinzani, Adama Barrow alishinda katika uchaguzi wa Rais wa Disemba Mosi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.