Rais Yahya Jammeh atangaza hali ya hatari Gambia
Rais Yahya Jammeh wa Gambia ametangaza hali ya hatari nchini humo kwa siku 90 akiashiria kuingiliwa na nchi ajinabi uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliofanyika mwezi Disemba mwaka jana.
Rais Jammeh ametamka hayo jana kupitia televisheni ya taifa. Baadhi ya nchi za eneo zimekuwa zikifanya jitihada za kumshawishi Rais Jammeh amkabidhi madaraka kiongozi wa upinzani Adama Barrow ambaye alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa tarehe Mosi Disemba mwaka jana. Barrow amepangiwa kuapishwa hapo kesho kama Rais mpya wa Gambia.
Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa hali hiyo ya hatari iliyotangazwa na Jammeh inaweza kuipelekea serikali kuakhirisha sherehe hizo za kumuapisha rais mpya. Mapema jana duru moja ya kijeshi ya Nigeria ilisema kuwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) imetishia kuingilia kijeshi huko Gambia iwapo Rais Jammeh atakataa kuondoka madarakani baada ya kumalizika muhula wake wa miaka mitano hii leo.