Rais Barrow atangaza makamu wake mwanamke akiwa Senegal
Rais mpya wa Gambia Adama Barrow amemteua kiongozi wa wanawake wa muungano wa upinzani uliomsaidia kuingia madarakani, kuwa makamu wake.
Hayo yametangazwa na msemaji wa Barrow, Halifa Sallah katika mazungumzo na waandishi wa habari hapo jana na kuongeza kuwa, Aja Fatoumata Tambajang, mwanaharakati na mpinzani wa muda mrefu wa utawala wa Yahya Jammeh, ndiye Makamu wa Rais wa Gambia.
Fatoumata Tambajang, ambaye amewahi kuwa afisa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, alitoa mchango mkubwa sana wa kuwashawishi viongozi wa upinzani nchini humo kuungana bega kwa bega kumuondoa madarakani Jammeh.
Sallah amebainisha kuwa, Barrow anatazamiwa leo Jumanne kuweka wazi majina ya watu watakaojaza nafasi katika baraza lake jipya la mawaziri.
Hapo jana Rais Barrow aliwataka askari wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS, kusalia nchini humo kwa lengo la kusimamia usalama na amani.
Aidha amewataka raia wa Gambia kushikamana na kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki muhimu cha kujiri mabadiliko ya kisiasa ndani ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika.
Rais Barrow angali katika nchi jirani ya Senegal ambako aliapishiwa kwa zaidi ya wiki moja sasa, licha ya kuondoka Gambia mtangulizi wake aliyeiongoza nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika kwa miaka 22, Yahya Jammeh.