Iran yataka kufanyika kikao cha dharura cha OIC kujadili kadhia ya Palestina
-
Sayyid Abbas Araqchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumza na kubadilishana mawazo na mwenzake wa Gambia, Mamadou Tangara, ambaye nchi yake ndiye mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), kuhusu matukio ya sasa huko Palestina hususan Ukanda wa Gaza.
Katika mazungumzo hayo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Gambia, Mamadou Tangara, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani njama hatari na za kijinai za Marekani na Wazayuni za kutaka kufuta kizazi na kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao na kusisitiza kuwa mpango huo ni wa kikatili na kinyume na kanuni na sheria zote za kimataifa. Sayyid Abbas Araqchi amesisitiza haja ya jamii ya kimataifa kupinga vikali njama hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria mashauriano yaliyofanywa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiarabu na Kiislamu, na ameiomba Gambia, ikiwa mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo, kufanya jitihada za kuitisha kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (kuhusu Gaza) haraka iwezekanavyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Gambia sanjari na kuishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kulitilia maanani suala la Palestina, amekaribisha pendekezo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran la kufanyika kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa OIC ili kujadili hali ya Palestina.
Mamadou Tangara amesisitiza kuwa atashauriana na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kuhusiana na suala hilo.