Kuongezeka mivutano kati ya Umoja wa Ulaya na Burundi
Hali ya mvutano kati ya Burundi na Umoja wa Ulaya ingali inaendelea na sasa serikali ya Bujumbura imeutuhumu umoja huo kuwa unakiuka mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo.
Katika hali ambayo Bunge la Ulaya wiki iliyopita lilipitisha azimio lililoituhumu serikali ya Burundi kuwa imekiuka haki za binadamu kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Hata hivyo msemaji wa serikali ya Burundi, Philippe Nzobonariba ameitaja hatua ya umoja huo kuwa haifai na kwamba ni mfano wa uingiliaji wa nchi za Magharibi katika masuala ya ndani ya Burundi. Msemaji wa serikali ya Bujumbura ameeleza kuwa, azimio hilo la Ulaya limepitishwa bila ya kuzingatia hatua chanya zilizochukuliwa na serikali ya nchi hiyo mkabala na wafanya maandamano na wapinzani wa kisiasa.
Philippe Nzobonariba amesema, azimio la Bunge la Ulaya limeandaliwa kwa kutegemea ripoti za Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu na Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Burundi na kwamba, wabunge wa Ulaya wamechukua uamuzi wa kiuhasama na kichochezi. Msimamo huo umechukuliwa ikiwa imepita miaka miwili tangu Burundi ikumbwe na mgogoro wa kisiasa. Mgogoro huo umesababisha mauaji na watu wengi nchini humo na kuwalazimisha maelfu ya raia wa nchi hiyo kuwa wakimbizi katika nchi jirani.
Chama tawala na askari usalama wa serikali ya Burundi wamekuwa wakikandamiza maandamano ya amani ya wapinzani serikali na kuwatia nguvuni wengi miongoni mwao. Ripoti zinasema kuwa, wapinzani wa serikali ya Bujumbura wanaendelea kukabiliwa na mashinikizo, mateso, kutiwa mbaroni na hata kuuawa. Hadi sasa kumechukuliwa hatua mbalimbali za kutafuta suluhu la mgogoro wa kisiasa nchini Burundi na mashauriano mengi yamefanyika katika uwanja huo. Hata hivyo juhudi hizo hazijaweza kuhitimisha mgogoro huo.
Wakati huo huo viongozi wa Burundi wamekanusha tuhuma za kutumiwa mabavu na kukanyaga uhuru wa kisiasa nchini humo. Serikali ya Bujumbura imelaani ripoti za taasisi za kimataifa na haki za binadamu zilizoashiria ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo. Viongozi wa Burundi pia waliwazuia kuingia nchini humo maripota na wakaguzi wa taasisi hizo za haki za binadamu. Si hayo tu, bali chama tawala nchini Burundi pia kimeifunga taasisi kongwe zaidi ya kutetea haki za binadamu nchini humo.
Hatua zote hizo zimechukuliwa huku taasisi za kimataifa zikiendelea kulaani ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika nchini Burundi na zinaendelea kufanya juhudi za kuishinikiza zaidi serikali ya Bujumbura. Kuhusiana na suala hilo Umoja wa Ulaya ukiwa mshirika muhimu zaidi wa kibishara wa nchi hiyo umeamua kuzidisha mashinikizo kwa viongozi wa Burundi na kuzungumzia uwezekano wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Hatua ya Umoja wa Ulaya ya kutolipa mishahara ya wanajeshi Burindi wa kulinda amani katika kikosi cha Umoja wa Afrika huko Somalia (AMISOM) pia imeifanya serikali ya Bujumbura iwaondoe wanajeshi wake huko Somalia.
Pamoja na hayo yote, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi wiki iliyopita aliagiza kuwaachia huru wafungwa wengi wa kisiasa. Japokuwa vifungo vya baadhi yawafungwa hao wa kisasa vinahusiana na matukio yaliyojiri Burundi kabla ya mwaka 2015, lakini weledi wengi wa mambo wameitaja hatua hiyo kuwa ni sawa na kulegeza kamba na kurudi nyuma serikali ya Bujumbura na katika juhudi zake za kuboresha hali ya mambo ya nchi hiyo.