Feb 06, 2017 12:32 UTC
  • Juhudi za nchi za Sahel kwa ajili ya kupambana na ugaidi

Viongozi wa nchi tano za eneo la Sahel zinazojumuisha Mauritania, Chad, Burkina Faso, Niger, Mali wamekutana katika kikao cha dharura kujadili hali ya usalama nchini Mali.

Matatizo ya kiusalama na harakati za makundi ya kigaidi  na yale yanayobeba silaha yamesababisha mgogoro mkubwa katika nchi za  Afrika hususan zile za eneo la Sahel. Kuwepo  makundi ya kigaidi kama Boko Haram, al Murabitun, al Qaida na mengineyo katika eneo hilo kwa miaka mingi sasa kumesababisha matatizo mengi na kuvuruga usalama na amani ya wakazi wa eneo hilo. Kwa mfano tu mashambulizi yanayofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria na katika nchi jirani hadi sasa yameua maelfu ya raia wasio na hatia na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Hali hiyo ya mauaji ya Boko Haram inashuhudiwa pia katika nchi kama Niger na Cameroon. Kundi hilo pia linatishia usalama wa nchi za Chad na Mauritania.

Magaidi wa mtandao wa al Qaida

Mbali na matatizo yanayosababishwa na harakati za  kundi la kigaidi la Boko Haram, nchi za Sahel na magharibi mwa Afrika pia zinasumbuliwa na athari mbaya za vita vya ndani huko Mali. Hali hiyo ya ukosefu wa amani katika nchi ya Mali inawatia wasiwasi viongozi wa nchi za eneo hilo kwamba yumkini ikatumiwa na makundi mengine ya kigaidi kama maficho salama na kituo cha kupanga na kuendeshea harakati zao katika nchi jirani.  

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram lenye makao yake nchini Nigeria 

Suala la kustawi kwa makundi ya kigaidi katika eneo hilo pia linaweza kuchunguzwa kwa pande kadhaa. Upande wa kwanza ni kuwa, makundi hayo yanataka kufaidika na utajiri na nafasi ya kistratijia ya nchi hizo. Kuongezeka magenge ya biashara za magendo na wahamiaji haramu ni moja ya njia zinazotumiwa na makundi hayo kujipatia fedha. Katika upande mwingine hata hivyo inaonekana kuwa aghalabu ya makundi hayo yanapewa msaada wa nyuma ya pazia na baadhi ya nchi ajinabi. Si tu kwamba ni nchi za Magharibi pekee ndizo zinazokodolea macho utajiri na maliasili za nchi hizo, bali  katika mpango  mpya wa kisiasa baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudi Arabia na pia utawala wa Kizayuni zinataka kuwa na ushawishi katika maeneo hayo; na hivyo kuyaimarisha makundi hayo ya kigaidi ili kufikia malengo yao. Ufaransa pia imepigania kuwepo vikosi vyake huko Mali kwa lengo hilo hilo. Ndio maana kushtadi kwa harakati na hujuma za makundi hayo hivi sasa kumegeuka na kuwa tishio kwa ulimwengu mzima. Nchi nyingi za eneo la Sahel katika miaka ya hivi karibuni zimeonyesha jitihada za kurejesha amani na uthabiti wa kisiasa katika eneo; na kwa msingi huo mwaka 2015 pia kulisainiwa makubaliano ya kusaka amani kati ya chama tawala na makundi mbalimbali ya upinzani na yale ya wanamgambo wanaobeba silaha huko Mali. Hata kama vipengee vya makubaliano hayo havijatekelezwa nchini humo huku mapigano  yakiendelea, lakini kujiri mashambulizi ya kigaidi na kuuliwa raia nchini humo ni kengele ya hatari kwa nchi zote za eneo la Sahel. Wakuu wa nchi za eneo hilo wamefanya kikao cha dharura lengo likiwa ni kuchukua hatua na kufikia msimamo thabiti wa pamoja wa kieneo  ili kuendesha mapambano ya pamoja dhidi ya makundi ya kigaidi. Hata hivyo tunapasa kusubiri na kuona ni kwa kiasi gani nchi hizo zitakuwa tayari kushirikiana kwa karibu katika mazingira ya hivi sasa, ambapo nchi za nje zimekuwa zikifanya kila juhudi kuingilia masuala yao ya ndani. 

Tags