Apr 26, 2017 13:03 UTC
  • Iran itakabiliana na vitisho vyote vya Marekani

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran itakabiliana na kila aina ya vitisho vya Marekani na madola mengine ya kibeberu.

Brigedia Jenerali Hussein Dehqan ameyasema hayo leo  mjini Moscow, Russia wakati akitoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Usalama.

Ameongeza kuwa, hatua za  nchi za Magharibi na hasa Marekani za kukiuka sheria ni jambo ambalo limehatarisha haki ya mataifa kuainisha hatima yao na kuwa na mamlaka ya ndani ya kujitawala.

Brigedia Jenerali Dehqan ameongeza kuwa, "Ulimwengu unakabiliwa na vitisho  vingi vya usalama kutokana na rais mpya wa Marekani kutowajibika katika tabia na matamshi yake. "Ameongeza kuwa rais huyo wa Marekani anahatarisha usalama wa dunia kwa kuimarisha ushirikiano na utawala wa Kizayuni wa Israel, Saudi Arabia na Israel katika kuunga mkono makundi ya magaidi wakufurishaji.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amekosoa pia utumizi wa sera za kindumakuwili katika taasisi za kimataifa wakati wa kukabiliana na mauaji ya watu wasio na hatia duniani. Amesema ulimwengu unahitaji azma imara katika kupambana kikamilifu na ugaidi sambamba na kuondoa sababu zote zinazopelekea kuibuka na kuenea ugaidi.

Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa Moscow  MCIS

Brigedia Jenenrali Dehqan ameongeza kuwa Iran inapinga kikamilifu uundwaji, urundikaji, na utumizi wa silaha za maangamizi ya umati na kuongeza kuwa, iwapo dunia itakuwa na irada katika kuupokonya utawala wa Israel silaha zake za nyuklia, basi usalama wa Mashariki ya Kati utadhaminiwa.

Waziri wa Ulinzi wa Iran aidha amesistiza kuhusu kuendelea ushirikiano wa Iran na Russia katika vita dhidi ya ugaidi na kusema: "Kwa ushindi wa Russia, Iran, na serikali ya kisheria na halali ya Syria dhidi ya magaidi,  eneo na dunia kwa ujumla itashuhudia amani."

Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Usalama wa Moscow umeanza leo Jumatano ambapo washiriki wanachunguza makundi ya magaidi wakufurushaji nchini Syria na Yemen na pia matukio mapya ya Mashariki ya Kati na dunia nzima kwa ujumla.

Tags