Dec 19, 2019 02:33 UTC
  • Mawaziri wa Ulinzi wa nchi za Afrika wakutana kujadili usalama na amani ya bara

Mawaziri wa Usalama na maafisa wengine wa ngazi za juu wa usalama wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanatazamiwa kukutana leo Alkhamisi kujadili masuala ya amani na changamoto za kiusalama zinazolikabili bara hilo.

Kamisheni ya Umoja wa Afrika imetoa taarifa ikisema, Mawaziri wa Ulinzi, wakuu wa majeshi na wakuu wa usalama kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanapanga kufanya mkutano wa ngazi ya juu hii leo kujadili masuala ya amani na usalama wa bara hilo.

Taarifa ya kamisheni hiyo ya AU imebainisha kuwa, kikao hicho cha usalama ni sehemu ya Mkutano wa 12 wa Kawaida wa Kamati Maalumu ya Kiufundi ya Ulinzi na Usalama (STCDSS).

Kwa mujibu taarifa hiyo, mkutano huo mbali na kutathmini na kujadili mambo ya amani na usalama kwa upande wa kutoa miongozo ya sera, utaangazia pia utendaji wa Kikosi cha Akiba cha Afrika ASF.

Ramani ya Afrika

Aidha wakuu hao wa ulinzi na usalama wa nchi za Afrika wanatazamiwa kujadili mikakati ya kuzuia migogoro katika nchi za bara hilo. Kadhalika wakuu wa usalama na ulinzi wa nchi 55 wanachama wa AU wanatazamiwa kujadili mpango wa kulifanya bara Afrika liwe thabiti kufikia mwaka 2063.

Magenge ya kigaidi kama vile Boko Haram, al-Shabaab na makundi waitifaki wa Daesh yamekuwa yakifanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Afrika na kuvuruga amani, usalama, uthabiti na maendeleo ya bara hilo.

Tags