Jun 22, 2024 11:18 UTC
  • Cuba kujiunga rasmi kwenye kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel ICJ

Cuba imetangaza kutuma ombi la kujiunga kwenye kesi ya Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaotenda jinai dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Cuba imesema katika taarifa ya jana Ijumaa kuwa, Havana itajiunga rasmi kwenye kesi ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Israel, kutokana na utawala huo wa Kizayuni kushadidisha mashambulizi yake dhidi ya watu wa Gaza.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa: Hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ukanyagaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Cuba sasa imejiunga na nchi nyingine kama vile Nicaragua, Colombia, Libya, Maldives, Misri, Ireland, Ubelgiji, Uturuki, na Chile ambazo zimetangaza rasmi kujiunga na mashtaka ya Afrika Kusini dhidi ya Israel katika makahama ya ICJ.

Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba amekuwa akiitetea wazi wazi Palestina

Januari mwaka huu pia, Bruno Rodríguez Parrilla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba alisema katika mkutano wa Harakati ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) huko Kampala, Uganda kuwa: Havana inaunga mkono kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini huko Hague kuhusu mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Wananchi wa Cuba wamekuwa wakiandamana mara kwa mara kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, sambamba na kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Aidha Rais Miguel Diaz-Canel wa nchi hiyo amenukuliwa mara kadhaa akisisitiza kuwa, mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza ni 'Holocaust' halisi na ya kweli.

Tags