Iran yataka Umoja wa Mataifa ulaani uchokozi wa Marekani na Israel
(last modified Tue, 01 Jul 2025 04:32:52 GMT )
Jul 01, 2025 04:32 UTC
  • Iran yataka Umoja wa Mataifa ulaani uchokozi wa Marekani na Israel

Katika barua rasmi iliyowasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Balozi Amir Saeid Iravani, siku ya Jumatatu ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kutambua Israel na Marekani kama wavamizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Balozi Iravani ameonya kuwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya kiraia ya Iran si tu yanahatarisha amani ya kimataifa, bali pia yanadhoofisha mfumo wa kutoeneza silaha za nyuklia, na yanakiuka haki ya msingi ya Iran ya kuendeleza matumizi ya nishati ya nyuklia kwa njia ya amani.

Akinukuu ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Iravani ameeleza kuwa Iran inaendelea kutimiza wajibu wake wa kisheria chini ya mikataba ya kimataifa, na hivyo mashambulizi hayo hayana msingi wowote wa kisheria wala wa kimaadili.

Amesisitiza kuwa: “Baraza la Usalama pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kuchukua hatua thabiti na za haraka kulinda heshima na uhalali wa taasisi hii ya kimataifa. Ukimya katika hali hii unaweza kufasiriwa kama kushirikiana kwa njia ya kutochukua hatua, jambo ambalo linatishia misingi ambayo Umoja wa Mataifa ulijengwa juu yake.”

Kutokana na uzito na athari za ukiukaji huu wa wazi wa sheria za kimataifa, Iran inaitaka Jamii ya Kimataifa kupitia Baraza la Usalama kufanya yafuatayo:

1.

Kulaani vikali hatua ya uchokozi isiyo halali inayofanywa na Israel na Marekani, kama uvunjaji wa Hati ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na Maazimio ya Baraza la Usalama nambari 2231 (2015) na 487 (1981).

2.

Kuziwajibisha Israel na Marekani kwa mujibu wa Sura ya Saba ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kamili kwa uharibifu uliosababishwa, na kuweka mikakati ya kuepusha marudio ya vitendo hivyo vilivyo kinyume cha sheria.

Aidha, Iran inatoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwasilisha taarifa rasmi kuhusu ukiukwaji wa Azimio 487 (1981) unaofanywa na Israel, hususan mashambulizi dhidi ya maeneo ya nyuklia yanayosimamiwa na IAEA.

Balozi Iravani ameongeza kuwa, Marekani pia inapaswa kuwajibishwa moja kwa moja kwa vitendo vyake vya uchokozi pamoja na ushiriki wake wa wazi katika uchokozi wa Israel dhidi ya Iran. Amesema kutoshughulikia suala hili kunatishia uhalali na mamlaka ya taasisi ya Umoja wa Mataifa, na kunaweka hatarini misingi ya haki, amani na usawa wa mataifa yote.