Chama cha Jacob Zuma chaungana na upinzani Afrika Kusini
(last modified Tue, 18 Jun 2024 02:36:53 GMT )
Jun 18, 2024 02:36 UTC
  • Chama cha Jacob Zuma chaungana na upinzani Afrika Kusini

Jacob Zuma Rais wa zamani wa Afrika Kusini amesema kuwa, chama chake kitaungana na muungano wa upinzani kushirikiana kuipinga serikali huku kikishikilia msimamo wake wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa bunge mahakamani.

Chama chake cha uMkhonto weSizwe (MK) kitaungana na kile cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na mwanasiasa machachari Julius Malema kilichoshinda viti 39 bungeni katika bunge jipya la Afrika Kusini.

Msemaji wa chama cha MK Nhla-mulo N-dhle-la amedai kuwa, licha ya matokeo ya uchaguzi huo kuchakachuliwa, vyama ambayo vitaunda muungano huo wa upinzani vilifanikiwa kupata asilimia 30 katika uchaguzi wa bunge na kulingana na msemaji huyo matokeo hayo yanawaweka katika nafasi nzuri ya kupigania ukombozi kamili wa kiuchumi wa wazalendo.

Siku ya Ijumaa MK ilisusia kikao cha kwanza cha bunge ambapo mpinzani mkuu wa Zuma, Cyril Ramaphosa alichaguliwa kuwa rais wa taifa hilo kwa muhula wa pili.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, aliyechaguliwa tena kwa muhula wa pili baada ya chama chake cha ANC kudhoofika na kupoteza wingi katika bunge, anatarajiwa kutangaza baraza la mawaziri jumuishi.

Chama cha ANC, ambacho kiliwahi kuongozwa na mwanasiasa wa kimataifa Nelson Mandela, kilitawala siasa za Afrika Kusini kwa miongo mitatu iliyopita hadi kilipopoteza wingi wake katika uchaguzi wa taifa na wa majimbo tarehe 29 Mei.

Chama hicho, ambacho kilikuwa kikipata zaidi ya 60% katika chaguzi zote tangu 1994, isipokuwa 2019, wakati ushindi wake ulipopungua hadi 57.5%, kilipata 40.18% tu ya kura katika uchaguzi wa mwaka huu.