Afrika Kusini imeanza kuwaondoa chini ya ardhi wanaochimba madini kinyume cha sheria
(last modified Wed, 20 Nov 2024 11:48:21 GMT )
Nov 20, 2024 11:48 UTC
  • Afrika Kusini imeanza kuwaondoa chini ya ardhi wanaochimba madini kinyume cha sheria

Wataalamu wa uokoaji wa Afrika Kusini wamefika katika mgodi wa Stilfontein nchini humo kuanza operesheni ya kuwatoa chini ya ardhi wachimba madini kinyume cha sheria.

Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) limeripoti kuwa timu iliyopewa jukumu la kusimamia zoezi hilo inaongozwa na Wessels Morweng. 

Operesheni hiyo ya uokoaji inafuatia mzozo kati ya wachimba migodi hao na polisi ambao umeendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Awali familia za wachimba madini hao haramu ziliwatuhumu maafisa husika wa serikali kuwa wamewatelekeza ndugu zao chini ya ardhi na kuzuia juhudi za kuwapatia chakula na maji.

Hata hivyo polisi ya Afrika Kusini jana ilieleza kuwa wachimba madini hao haramu hawajatelekezwa, bali walikataa kutoka ndani ya migodi iliyotelelekezwa wakiogopa kutiwa mbaroni. 

Jana Msemaji wa Polisi ya Afrika Kusini alieleza kuwa, wanajipanga kutekeleza zoezi la kuwaondoa ndani ya mgodi kama walivyoagizwa lakini kwa kuchukua tahadhari za usalama. 

Wakati huo huo  Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alisema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya operesheni iliyopewa jina la "Vala Umgodi" kote nchini humo ambayo inaendelea kupata mafanikio katika kukabiliana na shughuli haramu za uchimbaji madini nchini Afrika Kusini.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa