Araqchi: Wanaotoa silaha kwa Israel wanaishutumu Iran kutuma makombora huko Russia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Umoja wa Ulaya na Uingereza zinatumia mienendo inayokinzana dhidi ya Iran ambayo inafichua sera za undumakuwili na kukwepa wajibu wao wa kulinda haki za binadamu.
Katika ujumbe wake kwenye akaunti yake ya X jana Jumanne, Abbass Araqchi alikosoa mienendo ya kinafiki ya nchi za Magharibi kuhusiana na haki za binadamu na kuandika kuwa: "EU na Uingereza, bila kuwasilisha ushahidi wowote, zimeishutumu Iran kuwa inaipatia Russia makombora ya balestiki na zimeyaweka vikwazo mashirika yetu ya ndege na meli."
Araqchi amesema: "Wakati huo huo, kulingana na hati zilizowasilishwa mahakamani, vyombo vya habari vya Uingereza leo vinafichua kwamba nchi hiyo inaendelea kuuza kwa Israel silaha za vipuri, ikifahamu kikamilifu kwamba silaha zake na vipuri vya ndege za kivita za F-35 vinatumiwa na Israel katika ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, takwimu rasmi zinaonyesha kuwa kati ya Oktoba 7, wakati vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza vilipoanza, na mwisho wa Mei, Uingereza ilitoa leseni zaidi ya 100 za kuuza silaha na zana za kijeshi kwa Israel. Thamani ya mikataba hii haijawekwa wazi.
Araqchi ameandika: "Sababu iliyotolewa na Uingereza kuhalalisha suala hilo ni eti kudumisha uhusiano na Marekani na NATO. Mienendo hii kinzani inafichua sera za undumakuwili na kutowajibika kuhusu haki za binadamu."