Kuendelea vitendo vya uhasama vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran
(last modified Tue, 19 Nov 2024 13:37:44 GMT )
Nov 19, 2024 13:37 UTC
  • Kuendelea vitendo vya uhasama vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran

Katika kuendeleza hatua zake za kiuadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu ya jana tarehe 18 Novemba Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa na kuliwekea vikwazo Shirika la Meli la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo kwa kisingizio na madai yasiyo na msingi ya eti Iran kuingilia mzozo wa Ukraine.

Taarifa ya Umoja wa Ulaya imedai kuwa: Kuhamishwa ndege zisizo na rubani, makombora yaliyotengenezwa Iran, teknolojia na vipuri vinavyohusiana na Iran na kupelekwa Russia na kupatiwa makundi ya wabeba silaha yasiyo ya kiserikali huko Magharibi mwa Asia na kwingineko ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa. Jana hiyo hiyo pia serikali ya Uingereza nayo iliiweka katika orodha yake ya vikwazo Kampuni ya Usafiri wa Meli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa madai hayo hayo.

Hatua ya chuki ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si suala geni, na umoja huo umewahi kuchukua hatua hizo huko nyuma.

Mwezi uliopita, Umoja wa Ulaya uliyawekea vikwazo mashirika matatu ya ndege ya Iran Air, Mahan Air na Saha Air, kwa kisingizio cha madai yasiyo na msingi ya kuhusika kwa Iran katika mzozo wa Ukraine ya kutuma makombora ya balestiki nchini Russia.

Kile ambacho ni jambo jipya ni kwamba Umoja wa Ulaya unadai kupelekwa ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran hadi Russia na kuzitumia katika vita vya Ukraine, katika hali ambayo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amethibitisha kuwa, hakuna makombora ya balistiki ya Iran ambayo yamesafirishwa kwenda Russia.

 

Wakati huo huo, maafisa na viongozi wa Tehran na Moscow wamekanusha mara chungu nzima madai hayo na kuelezea kuwa hayana msingi wowote. Ukweli ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilichukua msimamo wa wazi kuhusiana na suala hili tangu kuanza kwa vita vya Russia na Ukraine.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kupinga vita hivyo daima imekuwa ikitangaza kwamba inaunga mkono ufumbuzi wa kisiasa kwa ajili ya kutatuliwa hitilafu kati ya Russia na Ukraine na kumaliza mizozo ya kijeshi.

Utendaji wa kimsingi na uliotangazwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mgogoro wa Ukraine haujabadilika kwa muda wa miaka miwili iliyopita, na kwa mtazamo huu, kurudiwa kwa madai kwamba, Iran inatuma makombora ya balistiki nchini Russia kunafanywa kwa malengo na matashi ya kisiasa ya baadhi ya nchi za Magharibi na na kiuhakika madai hayo hayana msingi wowote kabisa.

 

Kuhusiana na suala hilo, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akijibu na kuzungumzia uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuziwekea vikwazo meli za Iran, ameichukulia hatua hiyo ya Ulaya kuwa haina msingi wowote wa kisheria, kimantiki wala kimaadili.  Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza: Uhuru wa kusafiri baharini ni mojawapo ya kanuni za kimsingi za haki za baharini. Aidha ameeleza kuwa, wakati watu wachache wanapochukua maamuzi ya kibaguzi, matokeo ya uoni wao mfupi huwarudia wao wenyewe.

Kwa muktadha huo, vitendo vya chuki na uhasama vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, badala ya kuwa na msingi wa kisheria na sahihi, chimbuko lake ni misimamo ya undumakuwili na mtazamo potofu wa umoja huo kuhusu haki za binadamu. Katika hali ambayo, Umoja wa Ulaya unapuuza na kufumbia macho mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza na jinai za utawala huo dhidi ya Lebanon na hata unashiriki katika jinai hizo, unadai kwamba, unaunga mkono haki za binadamu nchini Ukraine.

Kimsingi, kuwekewa vikwazo vya kiuadui Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muendelezo wa mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon, kwa sababu kwa kuweka vikwazo vya kikatili umoja huo unajaribu kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isiunge mkono mhimili wa muqawama, na kwa upande mwingine, unajaribu kuishughulisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili isiwe na umakini katika kujibu kwa nguvu na uthabiti vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni.

Nukta nyingine ni kuwa, inaonekana Umoja wa Ulaya ambao umekuwa ukitoa nara na kaulimbiu za kuwa kwake tayari kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuweka vikwazo hivi dhidi ya Tehran unathibitisha kwamba, utendaji wake halisi mkabala na Iran ni wa kukabiliana na taifa hili.

Ismail Beqaei, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu amesema kuhusiana na hilo: "Inaonekana baadhi ya nchi za Ulaya zinatilia mkazo juu ya kuendelezwa mchakato na utendaji wa makabiliano ambao kimsingi hautamnufaisha yeyote."