Siku 1000 za vita vya Ukraine na mustakabali wake usiojulikana
Jumatatu ya juzi 18 Novemba, 2024, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya mkutano mjini New York, kwa mnasaba wa siku elfu 1000 za Vita vya Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy alihutubia mkutano huo akiwa mwenyekiti wa zamu wa baraza hilo na kusisitiza kwamba, vita vya Ukraine havihusiani tu na suala la usalama wa nchi hiyo au Ulaya, bali ni suala la amani na usalama wa kimataifa na kanuni za kimsingi za hati ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Siku ya 1,000 ya vita vya Ukraine ilitimia Jumanne ya jana, Novemba 19, katika hali ambayo, kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni, hasa ruhusa ya Magharibi kushambulia ndani ya ardhi ya Russia kwa kutumia silaha za Magharibi, kunavifanya vita hivyo kuwa na mustakabali uliogubikwa na giza.
Vita nchini Ukraine, vilivyoanza Februari 24, 2022, vimeacha hasara kubwa za kibinadamu na kiuchumi. Zaidi ya raia 11,000 wameuawa na karibu 25,000 kujeruhiwa. Hata hivyo idadi ya kweli ni zaidi ya hiyo.
Uharibifu wa miundombinu na uhamaji wa kulazimishwa wa takriban watu milioni 10 wa Ukraine, wakiwemo milioni 6.8 ambao wametafuta hifadhi katika nchi nyingine, ni miongoni mwa matokeo makuu ya vita hivi vya uharibifu.
Ardhi ya Ukraine pia imekuwa moja ya maeneo yaliyochafuliwa zaidi ulimwenguni kwa mabomu ya kutegwa ardhini. Kulingana na makadirio, ujenzi wa Ukraine unahitaji gharama ya dola bilioni 500 kwa miaka kumi. Wakati huo huo, kila pande mbili za vita, yaani Russia na Ukraine, zinadai kuwa zimesababisha hasara kubwa za kibinadamu na kuharibu kiasi kikubwa cha vifaa vya kijeshi vya upande mwingine.
Filihali inaonekana kwamba, kuna mabadiliko makubwa yanayotokea katika muelekeo wa vita vya Ukraine. Mabadiliko haya ambayo kubwa zaidi ni kuchaguliwa tena Donald Trump na kuanza kwa muhula wake wa pili kama rais kuanzia Januari 20, 2025, na mtazamo wake wa vita vya Ukraine pamoja na utendaji wake ambapo nchi za Ulaya zinazounga mkono Kiev, hasa Ujerumani, zimefikia natija hii kwamba, vita vya Ukraine havitaendelea kama ilivyokuwa huko nyuma.
Kwa kuzingatia ukosoaji mwingi na mkali wa Trump kwa sera ya Washington kuhusu vita vya Ukraine wakati wa kampeni zake za uchaguzi, hususan kutoa msaada wa kijeshi na silaha wenye thamani ya makumi ya mabilioni ya dola, wanachama wa NATO wa Ulaya wana wasiwasi juu ya sera ya serikali ya Trump kuhusiana na Ukraine.
Tukio jengine muhimu na lenye hatima ni hatua mpya na iliyoratibiwa ya Marekani pamoja na Uingereza na Ufaransa ya kutoa idhini ya kushambulia ndani ya ardhi ya Russia kwa kutumia silaha za Magharibi kama vile kombora la ATACMS la umbali wa kilomita 300, na makombora ya anga ya cruise ambayo inahesabiwa kuwa tukio jipya na hatari katika vita vya Ukraine.
Hatua ya serikali ya Biden ambaye baada ya takriban miezi miwili hatokuwa tena rais wa Marekani imechukuliwa baada ya maombi ya miezi mingi ya rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy ya kuitaka Marekani imruhusu kutumia makombora ya nchi hiyo kupiga maeneo ya ndani ya nchi ya Russia.
Kwa upande wake gazeti la Le Figaro la nchini Ufaransa limeripoti kuwa, baada ya White House kuiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani kupiga maeneo ya ndani ya Russia, nchi nyingine mbili za Magharibi yaani Ufaransa na Uingereza nazo zimeiruhusu Ukraine kutumia silaha zao kushambulia maeneo ya ndani kabisa ya ardhi ya Russia.
Mara kwa mara, rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amekuwa akiwaomba viongozi wa nchi za Marekani wamruhusu kutumia silaha wanazompa kushambulia viwanja vya ndege, vituo vya kuvurumishia makombora vya Russia pamoja na maghala ya silaha na vituo vya mafua vya Russia.
Hatua hiyo inaonesha kuweko mabadiliko ya kimsingi katika misimamo ya nchi tatu zenye ushawishi mkubwa ndani ya Jeshi la Nchi za Magharibi NATO yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa. Inaonesha wazi kuwa lengo la nchi hizo ni kuchochea vurugu na vita vya Ukraine. Nchi hizo zimeipa idhini Ukraine kutumia inavyotaka silaha inazopewa na nchi za Magharibi kupiga sehemu yoyote inayotaka ndani ya ardhi ya Russia.
Hata hivyo kutokana na onyo la Russia kwamba hatua hiyo ya nchi za Magharibi itapelekea Ukraine kuangamizwa kikamilifu na hata kutokomezwa kwake, Umoja wa Mataifa unataka kuzuiwa kushadidi hali hiyo.
Antonio Guterres, huku akijibu ripoti ya New York Times kwamba Rais Joe Biden wa Marekani ameidhinisha mashambulizi ndani ya ardhi ya Russia kwa kutumiwa makombora ya masafa marefu yaliyotengenezwa na Marekani, amesisitiza kuwa: 'Kuongezeka kwa vita nchini Ukraine lazima kuepukwe haraka iwezekanavyo.'
Hapana shaka kuwa, kuichochea Ukraine kunakofanywa nchi za Magharibi na hatua mpya katika uwanja huu na kung'ang'ania viongozi wa juu wa Kiev, hasa Volodymyr Zelensky, Rais wa Ukraine, kuendeleza vita kali na isiyo na matunda kutasababisha tu hasara zaidi za kibinadamu kwa Ukraine na kuzidisha uharibu kwa nchi hiyo.