Kolivand: Iran kutuma tani 10 za misaada kwa watu wa Lebanon
(last modified Wed, 20 Nov 2024 02:38:52 GMT )
Nov 20, 2024 02:38 UTC
  • Kolivand: Iran kutuma tani 10 za misaada kwa watu wa Lebanon

Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRCS) ameeleza kuwa shirika hilo hivi karibuni litatuma tani 10 za misaada mbalimbali iliyotolewa na wananchi wa Iran kwa ajili ya wenzao wa Lebanon.

Pir Hossein Kolivand ameashiria namna Mhimili wa Muqawama unavyopambana dhidi ya mashambulizi na hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina na Lebanon na kusema, vijana na wataalamu elfu 70 wa taaluma mbalimbali za misaada na matibabu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran wametangaza kuwa wako tayari kutumwa katika maeneo hayo ili kutoa msaada. 

Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran ameongeza kuwa, wananchi wa Iran hadi sasa wamechanga zaidi ya tumani bilioni 300 taslimu na kuzikabidhi kwa shirika hilo kwa ajili ya Kambi ya Muqawama; na misaada hiyo itatumwa kwa watu waliolazimika kuwa wakimbizi na walioathiriwa na mashambulizi na vita vya mauaji ya kimbari ya Israel.

Athari za vita vya Israel Ukanda wa Gaza 

Pir Hossein Kolivand amesema kuwa misaada yote iliyokusanywa kwa ajili ya waathirika wa vita na wakimbizi huko Lebanon na Palestina ni pamoja na dawa za matibabu, maziwa ya unga, bidhaa mbalimbali za chakula na mahitaji mengine muhimu.