Onyo la duru za kiusalama za Israel kwa Netanyahu
(last modified Tue, 19 Nov 2024 07:43:29 GMT )
Nov 19, 2024 07:43 UTC
  • Onyo la duru za kiusalama za Israel kwa Netanyahu

Duru za usalama za utawala wa Kizayuni zimemtumia ripoti waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netnyahu, na kumuonya kuhusu nguvu za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na wajibu wa kutodharau nguvu hizo.

Baada ya HAMAS kuongoza operesheni ya kishujaa ya Kimbunga cha al Aqsa na baada ya utawala wa Kizayuni kuanzisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya watu wasio na hatia huko Ghaza kwa msaada kamili wa madola ya Magharibi hasa Marekani na Uingereza zaidi ya mwaka mmoja nyuma; pande mbalimbali za kambi ya Muqawama ziliingia vitani kupambana na utawala wa Kizayuni na kuwasaidia ndugu zao Wapalestina. Matukio ya hivi karibuni katika vita vya Ghaza na Lebanon yameonesha kuwa makundi ya Muqawama ya Palestina na Lebanon yako imara huku udhaifu wa jeshi la utawala wa Kizayuni ukizidi kuonekana, siku baada ya siku.

Siku ya Jumapili ya tarehe 17 Novemba, 2024, Hizbullah ya Lebanon ilifanya operesheni 17 za makombora na droni kupiga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, vituo vya kijeshi, mikusanyiko ya wanajeshi Wazayuni na maeneo mengine muhimu na nyeti ya Israel. Katika operesheni hizo zilizotumia makumi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaani droni, harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imetwanga maeneo muhimu mno ya Israel karibu na kitongoji cha al Khiyam na kuzuia utawala wa Kizayuni kusonga mbele kusini mwa Lebanon.

Wanamapambano wa HAMAS

 

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimeripoti kuwa jeshi la Israel lina udhaifu na mapungufu mengi na limefeli katika vita vyake na Hizbullah. Vyombo hivyo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimekuwa vikiripoti kwamba jeshi la Israel limepigishwa magoti na Hizbullah ya Lebanon.

Hayo yanajiri katika hali ambayo makundi ya Muqawama ya Palestina huko Ghaza nayo yanaendelea kupambana kiume na jeshi katili za Israel ambalo linapata uungaji mkono kamili na wa kuchupa mipaka kutoka kwa Marekani. Wanamapambano wa Palestina wameendelea kupata mafanikio mbalimbali katika mapambano yao dhidi ya wanajeshi wa Israel kiasi kwamba hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni umeshindwa kufikia malengo uliyotangaza kuwa ndiyo sababu ya kuanzisha uvamizi wao wa tangu tarehe 7 Oktoba 2023 huko Ghaza.

Maafisa wa masuala ya usalama wa utawala wa Kizayuni wamemwandikia ripoti Benjamin Netanyahu na kumuonya kwamba, hata baada ya kuuawa shahidi kiongozi wa HAMAS, Yahya Sinwar, harakati hiyo ya Kiislamu ya Palestina iko imara na inaendelea na mapambano yake sambamba na kuzidi kutoa vipigo kwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni yakiwemo maeneo ya kaskazini mwa Ghaza ambayo Israel ilikuwa inadai kuwa imewamaliza kikamilifu wanamapambano wa Palestina kwenye eneo hilo.

Makomandoo wa Hizbullah ya Lebanon

 

Jenerali Herzi Halevi, mkuu wa majeshi ya utawala wa Kizayuni na Ronen Bar na David Barnea wakuu wa mashirika ya kijasusi ya Israel ya Shabak na Mossad wamemuonya Netanyahu kuwa, hakuna ishara zozote zinaoonesha kwamba HAMAS watalegeza misimamo yao kuhusu kusimamisha vita, kuachilia wafungwa na kurudi nyuma katika maeneo yao.

Hii ni katika hali ambayo, Basem Naim, Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palesina HAMAS amesema kuwa, harakati hiyo iko tayari kwa ajili ya makubaliano ya kusimamisha vita Ghaza na amemtaka rais mteule wa Marekani, Donald Trump auamrishe utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe jinai zake. 

Kiongozi huyo mwandamizi wa HAMAS amesisitiza pia kuwa, harakati hiyo inakaribisha mapendekezo yoyote yatakayopelekea kusimamishwa vita kikamilifu, kutoka wanajeshi wa Israel Ukanda wa Ghaza, kurejea wakimbizi, kubadilishana mateka na kuruhusiwa kuingia misaada ya kibinadamu ndani ya ukanda huo. 

Utawala wa Kizayuni umewaua kigaidi viongozi mbalimbali wa harakati za Muqawama kwa ndoto kuwa wataweza kuzimaliza nguvu harakati hizo lakini uhakika wa mambo umekuwa ni kinyume chake. Si tu harakati hizo hazijaweka silaha chini, lakini pia zimezidi kuwa imara siku baada ya siku na zinazidi kutoa vipigo kwa wanajeshi vamizi na makatili wa Israel.