Walebanon waandamana nje ya ubalozi wa Israel mjini Pretoria
(last modified Sun, 10 Nov 2024 06:50:35 GMT )
Nov 10, 2024 06:50 UTC
  • Walebanon waandamana nje ya ubalozi wa Israel mjini Pretoria

Raia wa Lebanon wanaoishi nchini Afrika Kusini wamefanya maandamano nje ya ubalozi wa Israel mjini Pretoria, wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni unaendeleza vita na mashambulizi ya kinyama dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Walebanon kutoka matabaka mbalimbali, jana (Jumamosi) jioni walishiriki maandamano hayo wakilalamika kwamba, hujuma za Wazayuni dhidi ya nchi yao zimekuwa zikitokea mara kwa mara kwa miongo kadhaa sasa.

Huku wakieleza dhamira yao ya kupinga utawala wa Israel unaoungwa mkono na Marekani, wananchi wa Lebanon wamebainisha kushindwa kwa vyombo vya kimataifa na serikali za dunia kuchukua hatua zozote za kuishinikiza Israel kusimamisha vita.

Baada ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas kutekeleza operesheni ya kihistoria ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ili kukabiliana na kukaliwa kwa mabavu Palestina kwa miongo kadhaa, utawala huo ghasibu ulianzisha vita vya kila namna dhidi ya Gaza na Lebanon ambavyo hadi sasa vimepelekea mauaji ya watu 46,500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Aidha Walebanon walioshiriki maandamano mjini Pretoria wamekariri wito wa Waafrika Kusini wa kutaka nchi hiyo ifunge ubalozi wa utawala wa Kizayuni na kukata uhusiano na utawala huo ghasibu.

Afrika Kusini yenyewe ni katika wakosoaji wakubwa wa mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza, na tayari inakwenda mbio na harakati za kujibisha Tel Aviv katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa jinai zake huko Gaza.