Mahakama ya Katiba ya Zimbabwe yapinga mashtaka dhidi ya Mugabe
Mahakama ya Katiba ya Zimbabwe imekataa mashtaka yaliyowasishwa na mwanaharakati Promise Mkwananzi dhidi ya kiongozi mkongwe wa nchi hiyo, Robert Mugabe kwamba alikiuka katiba wakati wa maandamano ya mwaka jana ya wananchi dhidi ya utawala wake na chama tawala cha ZANU-PF.
Promise Mkwananzi ambaye mwaka jana alisaidia kupanga maandamano ya wapinzani wa serikali dhidi ya serikali ya Mugabe amesema katika mashtaka hayo kwamba hatua na matamshi ya Mugabe wakati na baada ya maandamano ya wananchi ya mwaka jana vilidhoofisha usalama wa taifa na kutishia raia wa Zimbabwe.
Mkwananzi amesema pia kwamba, katika matamshi yake Mugabe alisema chama cha ZANU-PF kinadhibiti jeshi na polisi ya Zimbabwe jambo ambalo ni kinyume na katiba.
Hata hivyo majaji 9 wa Mahakama ya Katiba ya Zimbabwe wametupilia mbali kesi hiyo wakisema mwanaharakati Promise Mkwananzi hakufuata utaratibu sahihi wa kuwasilisha mashtaka. Wakili wa mwanaharakati huyo amekubali uamuzi huo lakini amesema kesi hiyo itawasilishwa tena mahakamani katika kipindi cha siku 30.
Wakati wa ghasia na maandamano makubwa zaidi kushuhidiwa nchini Zimbabwe dhidi ya Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo hapo mwaka jana, kiongozi huyo alisema kuwa, wakati wa vita vya ukombozi aliwaadhibu waasi kwa kuwaweka chini ya ardhi kama mapanya na kutishia kwamba, atafanya hivyo tena dhidi ya viongozi wa maandamano ya wapinzani.