Viongozi wa kidini nchini Rwanda waunga mkono upangaji uzazi
Viongozi wa kidini nchini Rwanda wamekutana katika mji mkuu Kigali kujadili njia za kuboresha afya ya uzazi.
Viongozi wa Kiislamu na Kikristo nchini humo chini ya mwavuli wa Baraza la Dini la Afya (RICH) wametoa wito wa upangaji uzazi ili kuboresha nguvukazi ya vizazi vijavyo.
Sheikh Ismael Maniriho, Afisa wa Masuala ya Dini katika Ofisi ya Mufti wa Rwanda amesema kuwa, Uislamu unaunga mkono upangaji uzazi akisisitiza kuwa, mwanamke anafaa kujifungua mtoto mwingine baada ya kipindi cha miezi 30 ya kunyonyesha, ikiwa ni njia mojawapo ya upangaji uzazi.

Amebainisha kuwa: "Uislamu unaunga mkono wanawake kutumia mbinu za kisasa za kupanga uzazi, madhali hazina madhara kwa miili na afya zao."
Naye Onesphor Rwaje, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Rwanda amesema kuwa, mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuhakikisha kuwa, upangaji uzazi haukinzani na haki za mwanamke.
Mwaka uliopita, Kanisa Katoliki nchini Rwanda liliwataka wafuasi wake wasitumie mbinu za kisasa za upangaji uzazi likisistiza kuwa, ni kinyume na mafundisho na itikadi za kanisa hilo.