Marekani, Ulaya zatuhumiwa kuunga mkono ugaidi Libya
Jenerali Khalifa Haftar wa Libya amezituhumu nchi kadhaa za Ulaya na Marekani kuwa zinaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Libya.
Katika mahojiano aliyofanyiwa na Radio ya Misri ya ON LIVE siku ya Jumamosi, Jenerali Haftar alisema, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Italia na Marekani ni washirika wa magaidi nchini Libya. Jenerali Haftar pia amefichua kuwa Uturuki imekuwa ikunga mkono magaidi Libya lakini akasema, "tuliwarejesha katika majeneza magaidi ambao Uturuki ilikuwa imewatuma Libya." Ameongeza kuwa, Uturuki itapata hasara kubwa kwa madhara iliyowasababishia watu wa Libya. Haftar alikuwa muitifaki wa dikteta Muammar Gaddafi lakini akajiunga na mapinduzi ya Walibya dhidi ya Gadaffi mwaka 2011.

Machafuko yamekuwa yakitawala Libya tokea muungano wa kijeshi wa NATO uingilie mwamko wa Libya wa mwaka 2011 ambao ulipelekea kupinduliwa na hatimaye kuuawa Gaddafi. Mwaka 2014 serikali mbili hasimu ziliundwa Libya moja ikiwa katika mji mkuu Tripoli na ya pili mashariki mwa nchi hiyo.
Jenerali Haftar yuko katika serikali iliyoko mashariki katika mji wa bandarini wa Tobrouk ambayo imekataa kuitambua serikali iliyoko Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.