Jeshi la Nigeria lawashambulia tena Waislamu wa nchi hiyo
Jeshi na Nigeria pamoja na polisi wa nchi hiyo kwa pamoja wamelishambulia jengo moja la Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo katika mji wa Katsina ulioko kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Ripoti zaidi zinasema kuwa, Waislamu kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio hilo huku hali ya baadhi yao ikiripotiwa kuwa mbaya.
Jengo hilo ni makazi ya Sheikh Yaqub Yahya mmoja wa wajumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky. Hilo si shambulio la kwanza nchini Nigeria dhidi ya vituo au majengo ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambayo ni ya wafuasi wa madhehebu ya Kishia nchini humo.
Wakati huo huo jana wanachuo waliandamana katika mji mkuu Abuja wakitaka kuachiliwa mara moja Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anayeendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama licha ya mhakama kutoa amri ya kuachia huru mwanaharakati huyo pamoja na mkewe.
Katika upande mwingine, familia ya Sheikh Ibrahim Zakzaky imemshtajki Mwanasheria Mkuu wa Nigeria kutokana na kutotekeleza amri ya mahakama ya kuachiliwa huru mwanaharakti huyo wa Kiislamu.
Ikumbukwe kuwa, Mwezi Disemba 2015, Sheikh Ibrahim Zakzaky alipigwa risasi na kukamatwa na jeshi la Nigeria baada ya jeshi hilo kuua kundi la Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo. Serikali ya Rais Muhammadu Buhari imekataa kutekeleza amri ya mahakama inayotaka Sheikh Zakzaky aachiliwe. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikikosoa ukandamizaji wa vyombo vya usalama vya Nigeria dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.