Mgogoro wa kisiasa Libya na kufutwa makubaliano ya Skhirat
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26098-mgogoro_wa_kisiasa_libya_na_kufutwa_makubaliano_ya_skhirat
Mgogoro wa kisiasa umechukua sura mpya nchini Libya baada ya bunge la nchi hiyo kubatilisha makubaliano ya Skhirat yaliyounda Baraza la Uongozi pamoja na Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez Sarraj.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 08, 2017 09:53 UTC
  • Fayez Sarraj, mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya
    Fayez Sarraj, mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya

Mgogoro wa kisiasa umechukua sura mpya nchini Libya baada ya bunge la nchi hiyo kubatilisha makubaliano ya Skhirat yaliyounda Baraza la Uongozi pamoja na Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez Sarraj.

Makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa na pande mbalimbali za Libya na kujulikana kwa jina maarufu la makublaiano ya Skhirat yalitiwa saini tarehe 17 Disemba 2015 kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa katika mji wa Skhirat nchini Morocco. Sherehe za kutiwa saini makubaliano hayo zilihudhuriwa pia na Martin Kobler, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya na lengo lake ni kukomesha mgogoro wa miaka mingi sasa wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Makubaliano hayo yalipasisha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa itakayotawala katika kipindi cha mpito hadi utakapofanyika uchaguzi mkuu mwaka mmoja tangu kuundwa kwake. Ilikubaliwa kuwa serikali hiyo isimamie uchaguzi huo. Muundo wa serikali hiyo ni kuwa na baraza la uongozi ambalo litaundwa na watu 9 ambao ni rais, manaibu watano na mawaziri watatu. Baada ya mazungumzo hayo, hatimaye kuliundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya na kuanza kufanya kazi. Hata hivyo tangu siku za awali kabisa za kuundwa kwake, wapinzani na makundi kadhaa ya kisiasa yalianza kuipinga na hadi leo hii yamekataa kuitambua rasmi.

Sekta ya mafuta nchini Libya

 

Si hayo tu, bunge la Libya nalo limekataa kuwapigia kura ya kuwa na imani nao, wajumbe wa baraza la uongozi la serikali hiyo ya umoja wa kitaifa. Baadhi ya makundi ya wapinzani yanaamini kuwa, mustakbali na hatima ya Libya lazima iamuliwe ndani ya nchi hiyo tena na wananchi wenyewe wa Libya. Kwa mtazamo wa makundi hayo, serikali ya umoja wa kitaifa imeundwa na wageni ambao hawana ridhaa ya wananchi. Mivutano hiyo imejitokeza katika hali ambayo, uchaguzi wowote nao hauwezi kufanyika bila ya kuweko utulivu na usalama wa kutosha. Hivyo waungaji mkono wa uamuzi wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya wanasema kuwa, kuundwa serikali hiyo lilikuwa jambo la dharura katika jitihada za kurejesha utulivu na amani na hatimaye kuitisha uchaguzi na kutoa fursa kwa wananchi ya kujiamulia mustakbali wao. 

Ijapokuwa tangu kuundwa kwake, serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imefanya juhudi nyingi za kurejesha amani na utulivu nchini humo, lakini imekuwa ikikwamishwa mara kwa mara na makundi ya ndani ya Libya, kuweko magenge ya kigaidi nchini humo na uingiliaji wa wazi na wa siri wa madola ajinabi hususan ya Magharibi. Hata mivutano ya ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa nayo imepelekea kukwama juhudi za Fayez Sarraj, mkuu wa baraza la uongozi la Libya za kufikia malengo aliyokusudia. Tarehe 19 Januari mwaka jana 2016, Fayez Sarraj alisema kuwa maamuzi wa baraza hilo hayakuzingatia maslahi ya taifa la Libya na aliamua kuyafuta. Alisema, baraza hilo ni kizuizi katika utekelezaji wa makubaliano ya Skhirat kama ambavyo pia linakwamisha juhudi za kupatanisha makundi mbalimbali ya Libya.

Makundi yenye silaha ni moja ya migogoro mikubwa hivi sasa nchini Libya

 

Kiujumla ni kwamba, hali nchini Libya bado si shwari. Nchi hiyo yenye serikali mbili moja ikiwa ni ile iliyoko Tobruk, kila leo inashuhudia kuongezeka mivutano baina ya makundi tofauti huku kila kundi likitaka kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo. Wachambuzi wa mambo wanazilaumu nchi za Magharibi kwa kutumia jeshi lao la NATO kufanya uharibifu mkubwa nchini Libya wakati wa kampeni za kumngóa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Jeshi la nchi za Magharibi NATO linalaumiwa kwa kuitelekeza Libya baada ya kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu na kueneza silaha nyingi mikononi mwa makundi tofauti hasimu, suala ambalo limepelekea kushtadi migogoro nchini humo hadi leo hii. 

Hata hivyo, juhudi za kuyapatanisha makundi mbalimbali ya Libya zinaendelea, ingawa hadi hivi sasa zimeshindwa kutatua mgogoro huo. Kwa kuzingatia hali hiyo, tunaweza kusema kwamba, hatua ya bunge la Libya ya kutangaza rasmi kufuta makubaliano ya Skhirat ni pigo jingine katika juhudi za kuyapatanisha makundi ya Libya na kurejesha amani na utulivu nchini humo.