Kuna uwezekano mwana wa Gaddafi kurejea madarakani nchini Libya
Gazeti la Ra'ayul-Yaum linalochapishwa mjini London, Uingereza limeandika kuwa kuna uwezekano Saiful-Islam Gaddafi, mwana wa kiume wa aliyekuwa dikteta wa Libya Muammar Gaddafi akarejea madarakani nchini humo.
Toleo la jana la gazeti hilo limeandika kuwa katika hali ambayo, baada ya kupita miaka sita ya mapinduzi na mgogoro wa Libya mipango yote ya kurejesha amani na usalama nchini humo imegonga mwamba, kuna uwezekano wa Saiful-Islam Gaddafi, mwana wa kiume wa Muammar Gaddafi kurejea madarakani nchini humo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, hatua zote zilizochukuliwa na nchi za Magharibi nchini Libya zimeshindwa; ya mwisho kabisa ikiwa ni ya kujaribu kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.
Ra'ayul-Yaum limeashiria ripoti ya jarida la Foreign Policy la Marekani ambalo limezitaka pande zote akiwemo Rais wa nchi hiyo Donald Trump zijenge imani mara hii kwa Saiful-Islam Gaddafi.
Imeelezwa kuwa Trump anaitakidi kwamba hali ya Libya ilikuwa bora zaidi katika zama za Muammar Gaddafi kuliko hivi sasa.
Libya ya sasa iko katika hali ambayo chochote kinawezekana kutokea nchini humo huku nchi za Marekani, Russia, Uingereza na Ufaransa zikiwa zimefikia uamuzi kwamba hali ya sasa ya nchi hiyo lazima ibadilike kwa sababu machafuko na mapigano yana taathira hasi kwa usalama na maslahi yake ya kiuchumi.
Tangu mwaka 2011 kufuatia uingiliaji kijeshi wa shirika la kijeshi la NATO uliopelekea kuangushwa utawala wa Gaddafi, Libya inaendelea hadi sasa kushuhudia machafuko, mapigano na hali ya mchafukoge.../