Malalamiko kuhusu marekebisho ya katiba nchini Mauritania
(last modified Mon, 13 Mar 2017 12:12:21 GMT )
Mar 13, 2017 12:12 UTC
  • Malalamiko kuhusu marekebisho ya katiba nchini Mauritania

Wafuasi wa kambi ya upinzani nchini Mauritania wamefanya maandamano wakipinga marekebisho ya katiba ya nchi hiyo.

Mitaa ya mji mkuu, Nouakchott imeshuhudia maandamano makubwa ya wafuasi wa vyama vya upinzani ambao wanalalamikia hatua ya serikali ya kufanyia marekebisho baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo.

Muswada wa kuifanyia marekebisho katiba ya Mauritania ulipasishwa siku kadhaa zilizopita katika Bunge la nchi hiyo na tayari umeanza kuchunguzwa na wawakilishi wa Baraza la Seneti la nchi hiyo. Iwapo muswada huo utapasishwa, sheria hiyo itafuta taasisi kadhaa muhimu za nchi hiyo kama Mahakama Kuu na Baraza la Seneti. Vilevile bendera ya nchi hiyo itafanyiwa mabadiliko. Mauritania ina Bunge na Baraza la Seneti ambalo wajumbe wake wanachaguliwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja.  

Rais wa Mauritania amesema lengo la kufanyika marekebisho hayo ni kuboresha katiba ya nchi na kufuta Baraza la Seneti. Hata hivyo kambi ya upinzani inapinga marekebisho hayo na inaamini kuwa, Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa nchi hiyo anafanya mikakati ya kubakia madarakani baada ya kipindi chake cha uongozi kumalizika. 

Mohamed Ould Abdel Aziz

Mauritania ina nafasi maalumu katika eneo la magharibi mwa Afrika na miezi kadhaa iliyopita ilifanikisha mazungumzo ya kumshawishi rais wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh kuondoka madarakani na kuepusha vita vya ndani nchi hiyo. Kutokana na nafasi hiyo Mauritania inakodolewa macho na baadhi ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia. Riyadh ambayo imefeli na kupata pigo kubwa katika siasa zake kwenye eneo la Mashariki ya Kati, sasa inataka kuwa na ushawishi katika nchi za Waislamu barani Afrika. Saudi Arabia inatumia mbinu ya kutoa misaada ya kifedha kwa nchi zinazolengwa Ili kufikia lengo hilo la kujipanua na kueneza satua na ushawishi wake. Katika mkondo huo, wiki chache zilizopita Riyadh ilitiliana saini mikataba ya ushirikiano wa kijeshi, kiusalama na kipelelezi na serikali ya Nouakchott. 

Itakumbukwa kuwa, nchi 10 kati ya 22 wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ziko barani Afrika. Hivyo Saudi Arabia inafanya mikakati ya kutaka kuwa na ushawishi barani Afrika kupitia njia ya kuwa na satua katika nchi za bara hilo wanachama wa Arab League.  

Image Caption

Alaa kulli hal, iwapo marekebisho ya katiba yatapasishwa nchini Mauritania hatua hiyo itathabitisha zaidi nafasi ya rais wa nchi hiyo na kuzidisha uwezekano wa kubakia mdarakani baada ya kipindi chake kumalizika. Wakati huo Saudia itakuwa na matumaini ya kuendelea kuwa na mshirika wa kutegemewa katika kueneza siasa zake za kutaka kujipanua zaidi katika maeneo ya magharibi mwa bara la Afrika. Rais Mohamed Ould Abdel Aziz ambaye anaongoza Mauritania kwa vipindi viwili mfululozo, haruhusiwi kugombea tena nafasi hiyo kwa mujibu wa katiba ya sasa.

Mivutano ya kisiasa imekuwa ikitokoka kwa muda sasa nchini Mauritania na inatazamiwa kupamba moto zaidi baada ya marekebisho hayo ya katiba. Muungano wa vyama 15 vya siasa unaopinga marekebisho hayo unaituhumu serikali ya nchi hiyo kuwa haina mwenendo wa kidemokrasia. Vyama hivyo pia vilisusia uchaguzi uliopita wa rais na hadi sasa havijatambua rasmi matokeo ya uchaguzi huo.          

Tags