Afrika yaanza kutengeneza dawa za kukabiliana na UKIMWI
Nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara zimepiga hatua muhimu kuelekea kujitegemea zaidi katika masuala ya afya kupitia hatua ya hivi karibuni zaidi ya kutengeneza dawa za kukabiliana na Virusi Vya Ukimwi, (VVU).
Imeelezwa kuwa, vifaa vya uchunguzi vimeanza kupatikana katika programu za kitaifa na dawa hizo zimenunuliwa kwa ajili ya Msumbiji.
Meg Doherty, Mkurugenzi wa Mpango wa VVU wa Shirika la Afya Duniani, WHO amesema, "ununuzi wa dawa za VVU zilizotengenezwa Afrika kwa ajili ya Msumbiji ni hatua muhimu kuelekea kuimarisha mifumo ya usambazaji barani Afrika. Hii itachangia matokeo bora ya kiafya kwa watu wanaoishi na VVU ambao wanahitaji upatikanaji wa dawa bila kukatizwa".
Maendeleo hayo yametajwa kuwa ni hatua kubwa kwa bara ambalo linabeba karibu asilimia 65 ya mzigo wa VVU duniani na kwa muda mrefu limekuwa likitegemea uagizaji wa dawa muhimu za kufifisha VVU, (ARVs) na vifaa vya kupimia. Lakini hali hiyo inaonekana imeanza kubadilika.
Virusi vya Ukimwi, VVU hudhoofisha kinga ya mwili, na kupunguza uwezo wake wa kupambana na maambukizi na aina fulani za saratani. Bila matibabu ya wakati, vinaweza kusababisha ugonjwa wa Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) ambayo ni hatua ya juu zaidi ya maambukizi.
WHO imesema mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi pana za kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani na kuboresha upatikanaji wa teknolojia muhimu za kiafya kote barani Afrika.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limekuwa likishirikiana na nchi, wazalishaji na mashirika, Mifuko ya afya duniani - ikiwemo Global Fund na Unitaid - ili kupanua uzalishaji wa Kiafrika wenye uhakika wa ubora.../