Sep 16, 2024 11:17 UTC
  • Kuendelea visa vya watu kujichoma moto huko Marekani; nembo ya kupinga vita vya Ukanda wa Gaza

Raia mmoja wa Marekani aliyejulikana kwa jina na Matt Nelson amejichoma moto katika mji wa Boston akipinga na kulalamikia vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza.

Huyo ni mtu wa nne nchini Marekani kuamua kujichoma moto akieleza upinzani wake dhidi ya vita na mauaji ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. 

Nelson alijichoma moto Jumatano tarehe 11 mwezi huu nje ya Hoteli ya Four Seasons mbele ya ubalozi mdogo wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Boston. Raia huyo wa Marekani ameamua kujichoma mota akipinga mauaji ya kimbari ya karibu Wapalestina elfu 50 yaliyofanywa na jeshi la Israel ikishirikiana na Marekan katika vita vya sasa dhidi ya Ukanda wa Gaza. Nelson alisema katika video aliyoirusha hewani kabla ya kujitia moto kwamba: "Jina langu ni Matt Nelson na ninataka kuchukua hatua kali ya upinzani. Sote tunabeba dhima mkabala wa mauaji ya kimbari yasiyo na kikomo yanayofanyika huko Gaza." Amesema, lengo la kuonyesha upinzani na malalamiko yake ni kuitaka serikali ya Marekani iache kutoa misaada ya kifedha na silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel; misaada ambayo utawala huo unaitumia kuwafunga jela na kuwaua Wapalestina wasio na hatia.

Nelson pia ametoa wito wa kuwekewa mashinikizo utawala wa Kizayuni ili usitishe mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Raia huyo wa Marekani  amezitolea wito nchi mbalimbali ziunge mkono uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na maafisa wengine wa utawala wa Kizayuni, na kusisitiza kuwa: "Inatarajiwa kwamba demokrasia itahudumia irada na matakwa ya wananchi na si kwa ajili ya kutumikia maslahi ya matajiri. Tumia nguvu na uwezo wako na ikomboe Palestina."

Kabla ya Nelson kujichoma moto, raia wengine watatu wa Marekani walikuwa tayari wamejichoma wakilalamikia vita vya Marekani na Israel dhidi ya Gaza, jinai za utawala wa Kizayuni na uungaji mkono wa pande zote wa serikali ya Biden kwa Israel. 

Aaron Bushnell, Mmarekani aliyejichoma moto kupinga vita vya Gaza

Miongoni mwa visa vikuu vya kujichoma moto raia wa Marekani wanaopinga kuendelea vita huko Gaza na sera za serikali ya Marekani za kuiunga mkono Israel, tunaweza kuashiria kujichoma moto Aaron Bushnell, askari wa jeshi la anga la Marekani aliyekuwa na umri wa miaka 25 Jumapili mchana Februari 25 mwaka huu. Bushnell alijichoma moto  mbele ya ubalozi wa Israel huko Washington akipinga mauaji ya kimbari ya Israel katika vita vya Gaza. Hatua hiyo ni miongoni mwa kadhia zilizoakisiwa pakubwa na vyombo vya habari duniani, ambapo walimwengu wameweza kutambua wazi mateso na masaibu ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. 

Bushnell alisema katika hotuba yake aliyoirusha mtandaoni huku akiwa amevalia sare za jeshi kwamba "sitaki kushiriki tena katika mauaji ya kimbari." Baada ya hapo, alijimwagia mafuta na kujichoma mota huku akipaza sauti akisema "Palestina ikombolewe, Palestina ikombolewe." Masaa machache kabla ya kujichoma moto, Aaron Bushnell alikuwa ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa:" Wengi kati yetu tunapenda kujiuliza kwamba, kama ingekuwa katika zama za utumwa ningechukua hatua gani kama ningelikuwa hai? Je, ningetekeleza sheria za Jim Crow au zile za ubaguzi wa rangi? Ningefanya nini ikiwa nchi yangu ingetekeleza mauaji ya kimbari? Jibu ni kuwa mnafanyya mauaji yya kimbari hivi sasa." Maneno ya mwisho ya Bushnell yalikuwa kama ifuatavyo: "Nakaribia kuchukua hatua kali ya upinzani. Lakini si hatua ya uchupaji mipaka ikilinganishwa na kile kinachowasibu wananchi wa Palestina katika makucha ya Maghasibu Wazayuni. Hili ni suala ambalo uongozi wetu umeamua kuwa ni jambo la kawaida."  

Vita vya umwagaji damu katika Ukanda wa Gaza vimeingia katika mwezi wa kumi na mbili sasa, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya mashahidi wa Kipalestina, ambao wengi wao ni watoto na wanawake, ni zaidi ya 41,000,  majeruhi wakiwa zaidi ya 95,000 na sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza pia ikiwa imebomolewa na kuharibiwa kikamilifu. Wakati huo huo vita vya Gaza vinahesabiwa kuwa moja ya maafa mabaya zaidi ya binadamu kuwahi kushuhudiwa duniani huku Wapalestina zaidi ya elfu 10 wakiwa hawajulikani walipo, mbali na vita hivyo kusababisha  maafa makubwa na kusababisha njaa iliyouwa mamia ya watoto wa Kipalestina katika eneo hilo.  

Israel imeuwa maelfu ya watoto wa Kipalestina Ukanda wa  Gaza 

Bila shaka jinai hizi za kutisha zisingewezekana bila msaada mkubwa wa kijeshi na silaha wa Marekani, nchi ambayo ilipeleka takriban tani 50,000 za silaha na zana nyingine za kivita kwa Israel. Licha ya kwamba nchini Marekani kumekuwa kukishuhudiwa maandamano makubwa ya wananchi hasa wanafunzi wa vyuo vikuu na hata wafanyakazi wa taasisi za nchi hiyo kama Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Wizara ya Usalama wa Taifa, pamoja na wasomi na wanafikra wa nchi hiyo kupinga sera ya uungaji mkono ya serikali ya Biden kwa utawala wa Israel, lakini White House inaendelea kuupatia silaha utawala wa Kizayuni. Hasa ikitiliwa maanani kuwa, nchi nyingine za Magharibi pia zimeendeleza uhusiano wao wa kibiashara na kijeshi na kiuchumi na hata wa kijeshi na Tel Aviv licha ya kutoa matamko tu ya kidhahiri ya kulaani jinai za Israel, na kwa utaratibu huo wanautia kiburi na kuusaidia utawala wa Kizayuni kuendelea na jinai zake huko Gaza. 

Tags