Vyombo vya habari vya michezo duniani vyalalamikia kimya cha FIFA mbele ya jinai za Israel
Aghalabu ya vyombo vya habari mashuhuri vya michezo duniani vimekosoa kimya, mchezo wa kisiasa na unafiki wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mkabala wa jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel.
Shirika la habari la Fars limearifu kuwa, vyombo vya habari vya michezo vya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani vimeeleza kuwa vyombo vya habari vyenye itibari vinailaumu na kuikosoa FIFA kwa kuchelewa kuchukua maamuzi ya kuiwekea vikwazo timu za soka za utawala wa Israel.
Shirikisho la Soka la Palestina mwezi Machi mwaka huu liliiandikia barua FIFA likitaka kuzuiwa kushiriki klabu za soka za Israel na timu ya taifa ya utawala huo katika michuano ya kimataifa.
Barua hiyo ililitaka pia Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuchukua hatia dhidi ya klabu za utawala wa Israel ambazo zinajishughulisha katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Licha ya kushtadi mapigano na vita katika eneo la Asia Magharibi, lakini vikao vya kufuatia na kushughulia changamoto hii ya kisheria vimeahirishwa mara kadhaa.
FIFA ilipanga tarehe 20 Julai mwaka huu kuitisha kikao cha dharura cha kuchunguza ombi la Shirikisho la Soka la Palestina lililotaka kuwekea vikwazo timu ya mpira ya wa miguu ya utawala wa Kizayuni; hata hivyo kikao hicho kimeakhirishwa hadi baada ya Agosti 31.
Zaidi ya Wapalestina elfu 40 wameuawa na karibu laki moja kujeruhiwa katika mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel.