Safari ya Pezeshkian nchini Russia na mahudhurio ya kwanza rasmi ya Iran katika BRICS
(last modified Tue, 22 Oct 2024 09:12:31 GMT )
Oct 22, 2024 09:12 UTC
  • Safari ya Pezeshkian nchini Russia na mahudhurio ya kwanza rasmi ya Iran katika BRICS

Mkutano wa 16 wa wakuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya BRICS umeanza leo katika mji wa Kazan nchini Russia. Rais Masoud Pezeshkian wa Iran anahudhuria mkutano huo unaotarajiwa kuendelea hadi 24 Oktoba.

Kundi la BRICS lilianzishwa huko Yekaterinburg, Russia mnamo 2009 kwa ushiriki wa Brazil, Russia, India na Uchina. Mwaka 2010 Afrika Kusini ilijiunga na kundi hilo na baadaye jina la kundi hilo lilibadilishwa kutoka BRIC na kuwa BRICS.  Misri, Ethiopia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) pia zilijiunga na jumuiya hiyo tangu mwanzoni mwaka huu.

Russia ilichukua uwenyekiti wa kiduru wa mwaka mmoja wa kundi la BRICS tangu Januari 1, 2024, na chini ya usimamizi wake, BRICS itafanya zaidi ya matukio 250 yanayohusu mada mbalimbali katika Mkutano wa Kazan. Mapema mwezi huu, Rais Putin alisema kuwa, kupitia uenyekiti wa nchi yake wa kundi la BRICS mwaka huu, kundi hilo linalenga kuongeza nafasi yake katika mfumo wa fedha wa kimataifa, kuendeleza ushirikiano kati ya benki, kupanua matumizi ya sarafu za nchi wanachama wa BRICS, na pia kuimarisha ushirikiano kati ya mashirika ya kodi na ushuru.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ilijiunga rasmi na kundi la BRICS tangu mwanzoni mwaka huu, inashiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano wa kilele wa kundi hili ikiwa ni mwanachama kamili. Kushiriki Rais Pezeshkian katika kikao cha BRICS ni sisitizo jingine la Iran la kustawishwa ushirikiano wa pande nyingi katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kazem Jalali, balozi wa Iran nchini Russia amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anashiriki kwa mara ya kwanza kikao cha wakuu wa nchi za BRICS  Iran ikiwa mwanachama rasmi, jambo ambalo ni nukta muhimu katika mwelekeo wa kustawisha ushirikiano wa pande nyingi wa nchi yetu. Mbali na viongozi wa nchi za BRICS, viongozi na maafisa wa ngazi za juu kutoka zaidi ya nchi 30 na mashirika ya kimataifa pia wanashiriki katika mkutano huu.

 

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa, kupambana na ukiritimba wa sarafu ya dola katika mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi wanachama wa BRICS kuna manufaa kwa pande kadhaa. Mosi ni kwamba jambo hilo linazidisha uhuru wa kundi hilo katika maamuzi yake hasa ya kiuchumi. Pili jambo hilo litaipelekea kila nchi mwanadhama wa BRICS kupunguza mno kutegemea Magharibi na kujiepusha na hatari za kifedha zinazosababishwa na utegemezi huo. Na tatu jambo hilo litafanikisha malengo ya BRICS ya kujiweka mbali na madola ya Magharibi na kutia nguvu madola ya Mashariki mwa dunia. Mohsen Rui Sefat, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: “Ni jambo lisilo na shaka kwamba moja ya shabaha kuu za BRICS ni kutia nguvu madola ya Mashariki mbele ya madola ya Magharibi na moja ya mambo ya lazima kabisa ya kufanikisha jambo hilo ni kupunguza kutumia sarafu za madola ya Magharibi katika mabadilishano yao ya kibiashara.”

Tab’an juhudi za kupambana na ukiritimba wa sarafu ya dola zilianza zamani, na kinachofanywa na kundi la BRICS hivi sasa ni kutia nguvu tu jitihada hizo.

Hapana shaka kuwa, kutumiwa sarafu za kitaifa katika mabadilishano ya kibiashara kutazuia kudharauliwa sarafu ya nchi yoyote ile na wakati huo huo kutaizuia Marekani kutumia sarafu yake ya dola kama silaha za kuzishinikiza nchi nyingine katika miamala ya kibiashara na mahusiano ya kiuchumi na kifedha bali hata katika masuala ya kiusalama. Tunaweza kusema pia kuwa, kundi la BRICS limefanya jambo la busara sana kuamua kutumia sarafu za nchi wanachama kwenye mabadilishano ya kibiashara hasa katika kupambana na ukiritimba wa madola ya Magharibi katika masuala ya kifedha ulimwenguni.