Magaidi 95 wa kundi la al-Shabaab wauawa Somalia
(last modified Tue, 22 Oct 2024 07:06:12 GMT )
Oct 22, 2024 07:06 UTC
  • Magaidi 95 wa kundi la al-Shabaab wauawa Somalia

Wizara ya Ulinzi ya Somalia imesema kwamba, jeshi la nchi hiyo likisaidiwa na washirika wa ndani na wa kimataifa, limefanya operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la wanamgambo wa al-Shabaab, na kuua wanachama zaidi ya 95 wa genge hilo la kigaidi.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Jeshi la Kitaifa la Somalia (SNA) limefanya operesheni kabambe huko Shabelle ya Kati, Galgadud, na mkoa wa kaskazini ya kati wa Mudug.

Luteni wa Kwanza Sheikh Abukar Mohamed, msemaji wa wizara hiyo, alisema katika mkutano na vyombo vya habari mjini Mogadishu Jumatatu jioni kwamba, magaidi 45 waliuawa na vijiji vitatu vilikombolewa wakati wa operesheni ya kijeshi huko Shabelle ya Kati.

Katika operesheni nyingine katika eneo la Galgadud katika jimbo la kati la Galmudug, magaidi 50 zaidi wa al-Shabaab waliuawa na vijiji vitano vikachukuliwa toka mikononi mwa kundi hilo la kigaidi.

Ikumbukwe kuwa, Oktoba 10, Wizara ya Habari ya Somalia ilitangaza kwamba magaidi 59 wa al-Shabaab na wanajeshi wanne waliuawa wakati wa operesheni za kijeshi katika mikoa ya kusini na kati ya Somalia.

Wanajeshi wa Somalia wakiwawinda magaidi wa a-Shabaab

Jeshi la Somalia huku likiungwa mkono na wanamgambo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na washirika wao wa kimataifa limekuwa likiendesha oparesheni mbalimbali na mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya al Shabaab tangu mwaka 2022. 

Hivi karibuni, Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kilikabidhi rasmi kambi ya kijeshi ya Kuday kwa vikosi vya usalama vya Somalia, kuashiria hatua muhimu katika awamu ya tatu ya uondoaji wa wanajeshi hao wa kigeni katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Tags