Rais wa Iran: Marekani na nchi za Ulaya ni watetezi wa uhalifu dhidi ya binadamu
(last modified Tue, 22 Oct 2024 15:26:04 GMT )
Oct 22, 2024 15:26 UTC
  • Rais wa Iran: Marekani na nchi za Ulaya ni watetezi wa uhalifu dhidi ya binadamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Nchi za Ulaya na Marekani zimeupatia silaha kwa nguvu zote utawala wa Israel na zinatetea jinai dhidi ya binadamu bila haya wala kuona soni.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, leo Jumanne alikuwa mgeni wa kwanza kufika katika ofisi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) mjini Tehran kutoa salamu za rambirambi kufuatia kuuawa shahidi Yahya Al-Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo, na kukutana na Khaled Qadoumi, mwakilishi wa Hamas nchini Iran.

Rais Pezeshkian amewaambia waandishi habari kwamba, nchi na madola yanayodai kutetea haki za binadamu na sheria za kimataifa zinakiuka sheria na haki zote, na kuongeza kuwa: Nchi hizo zinapigana na watu na zinauunga mkono utawala uliowafukuza watu wanaopigania haki na ardhi yao kutoka kwenye makazi yao. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Nchi za Ulaya na Marekani zimeipatia Israel silaha kwa nguvu zao zote na kutetea jinai zote dhidi ya binadamu bila haya; Hii inaonyesha kwamba nchi hizi zinaendeleza dhulma na uonevu duniani.

Rais Masoud Pezeshkian

Pezeshkian ameongeza kuwa: Vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza havitamalizika kwa kuua mtu mmoja au zaidi, lakini vinaweza kumalizwa kwa kutekelezwa uadilifu na kuzingatia haki za binadamu za pande zote, sio kwa kutumia dhulma na mauaji.

Akijibu swali kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Iran, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema: Shambulio lolote litapata jibu lake mwafaka.