Iran na Zimbabwe kuendeleza ushirikiano wa kibiashara
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, ameonana na mkuu mtendaji wa taasisi ya ustawi wa kibiashara ya nchi hiyo na pande mbili zimesisitizia haja ya kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi baina yao.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Ahmad Erfanian, balozi wa Iran chini Zimbabwe leo ameonana na mkuu huyo mtendaji wa taasisi ya ustawi wa kibiashara ya Zimbabwe mjini Harare na kusema kuwa, uhusiano mzuri wa kisiasa uliopo baina ya Iran na Zimbabwe ni fursa nzuri ya kuongezwa kiwango cha mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara baina ya nchi mbili.
Balozi wa Iran nchini Zimbabwe aidha amesema, Tehran na Harare zina fursa nyingi nzuri za ushirikiano na kusisitiza kuwa Iran iko tayari kushirikiana na Zimbabwe katika nyuga zote zikiwemo za sekta ya mafuta, madawa, vifaa vya kilimo, mada za kemikali, vifaa vya ujenzi na bidhaa za chakula.
Kwa upande wake, Bi Sithembile Pilime mkuu mtendaji wa taasisi ya ustawi wa kibiashara ya Zimbabwe ameishuruku Iran kwa kuwa pamoja na wananchi wa Zimbabwe katika hali zote na kuongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba nafasi ya Iran katika sekta ya biashara na uchumi nchini Zimbabwe haijafikia kiwango kinachotakiwa na kwamba Harare inayakaribisha mashirika ya Iran kutumia vizuri soko la Zimbabwe.
Aidha amesifu juhudi zinazochukuliwa katika kufanyia uchunguzi uwezo wa pande mbili wa kuweza kushirikiana ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuwa na uhusiano mzuri wa kibenki.