UN: Idadi ya waliopoteza maisha kutokana na malaria Burundi yapindukia 4000
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27034-un_idadi_ya_waliopoteza_maisha_kutokana_na_malaria_burundi_yapindukia_4000
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, idadi ya watu walioaga dunia kutokana na mripuko wa ugonjwa wa malaria nchini Burundi imeongezeka na kupindukia watu 4000, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2017 22:42 UTC
  • UN: Idadi ya waliopoteza maisha kutokana na malaria Burundi yapindukia 4000

Umoja wa Mataifa umesema kuwa, idadi ya watu walioaga dunia kutokana na mripuko wa ugonjwa wa malaria nchini Burundi imeongezeka na kupindukia watu 4000, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.

Ofisi ya Kushughulikia Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi imesema kuwa, mbali na watu elfu nne kuaga dunia kutokana na ugonjwa huo, kesi zaidi ya milioni 9 za ugonjwa huo unaoambukizwa na mbu zimeripotiwa nchini humo, kati ya Januari mwaka jana hadi hivi sasa. Ifahamike kuwa Burundi ina idadi ya watu  wapatao milioni 11. 

Takwimu hizo za kuogofya za Umoja wa Mataifa zimetolewa wiki mbili baada ya serikali ya Bujumbura kutangaza kuwa, watu 700 wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita nchini Burundi.

Ugonjwa wa malaria unasababishwa na mbu jike aina ya 'anopheles'

Waziri wa Afya nchini Burundi, Dakta Josiane Nijimbere amesema kuwa, tangu Januari Mosi hadi Machi 10 mwaka huu, watu zaidi ya milioni moja na laki nane wameugua malaria, ambapo 700 miongoni mwao wamepoteza maisha, ikiwa ni wastani wa watu 10 kila siku.

Serikali ya Burundi imesema, inahitaji dola milioni 31 za Marekani ili kukabiliana na mripuko huo wa malaria, unaotokea wakati huu ambapo nchi hiyo inakabiliwa na baa la njaa na migogoro ya kisiasa na kiusalama.