Wahajiri zaidi ya 150 waokolewa katika pwani ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27246-wahajiri_zaidi_ya_150_waokolewa_katika_pwani_ya_libya
Msemaji wa jeshi la majini wa Libya amesema kuwa, wahajiri zaidi ya 150 wameokolewa katika pwani ya nchi hiyo katika bahari ya Mediterania.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 03, 2017 22:59 UTC
  • Wahajiri zaidi ya 150 waokolewa katika pwani ya Libya

Msemaji wa jeshi la majini wa Libya amesema kuwa, wahajiri zaidi ya 150 wameokolewa katika pwani ya nchi hiyo katika bahari ya Mediterania.

Ayoub Qassim ametangaza kuwa walinzi wa pwani ya Libya wamewaopoa majini wahajiri zaidi ya 157 katika oparesheni mbili zilizofanywa Jumamosi na Jumapili hii karibu na pwani ya miji ya Zawiya na Sabrata iliyoko umbali wa kilomita takriban sabini au sabini na tano magharibi mwa Tripoli mji mkuu wa Libya.

Afisa huyo wa Libya ameongeza kuwa wahajiri hao waliokolewa wakati wakijaribu kuelekea barani Ulaya kwa njia zilizo kinyume cha sheria kupitia bahari ya Mediterania. 

Wahajiri haramu walionusurika kifo 

Msemaji wa jeshi la majini la Libya ameongeza kuwa, raia kutoka Syria, Morocco, Pakistan, Ghana, Sudan, Algeria na Niger ni miongoni mwa wahajiri hao haramu walionusrurika kufa maji. Shirika la Kimataifa la Wahajiri limesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kuwa, wahajiri 1037 wameokolewa majini kandokando ya pwani ya Libya katika kipindi cha wiki mbili zilizopita yaani kuanzia tarehe 16 hadi 30 mwezi Machi. Serikali ya Libya haiwezi kudhibiti mipaka yake ya majini na ardhini kutokana na machafuko yanayoisibu nchi hiyo na pia kuweko makundi mbalimbali ya kigaidi; kiasi kwamba nchi hiyo sasa imekuwa kituo kikuu cha kuanzia safari za maelfu ya wahajiri na wahamiaji kuelekea Ulaya.