Magaidi wa Boko Haram washadidisha mashambulio nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27468-magaidi_wa_boko_haram_washadidisha_mashambulio_nchini_nigeria
Watu kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulio mawili yaliyofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 08, 2017 11:18 UTC
  • Magaidi wa Boko Haram washadidisha mashambulio nchini Nigeria

Watu kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulio mawili yaliyofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Polisi ya Nigeria imetangaza kuwa watu watano wamejeruhiwa katika shambulio la mripuko wa bomu uliotokea leo asubuhi katika mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa Polisi ya Borno ameeleza kuwa mnamo majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri kwa saa za eneo hilo washambuliaji wawili wa kujitoa mhanga wanawake walitaka kuvamia msikiti ulioko karibu na mahakama kuu ya federali katika mji wa Maiduguri lakini wakatambulika kabla ya kuingia msikitini humo, hata hivyo mmoja wao alifanikiwa kufyatua kitufe cha mada za miripuko alizojifunga.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Polisi, katika mripuko huo washambuliaji hao waliuawa na watu wengine watano walijeruhiwa.

Wakati huohuo watu wenye silaha ambao ni wafuasi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, alfajiri ya kuamkia leo walivamia na kushambulia kijiji cha Wajiko katika jimbo la Borno. Katika shambulio hilo wanajeshi watano walijeruhiwa vibaya na wengine wanne walikamatwa matekwa.

Jeshi la Nigeria limethibitisha habari hiyo na kutangaza kuwa kituo cha wanajeshi katika kijiji hicho cha Wajiko kiliteketezwa kwa moto.

Tangu mwaka 2009 hadi sasa, zaidi ya watu 20,000 wameuawa nchini Nigeria katika mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram na wengine zaidi ya milioni mbili na laki tano wamepoteza makazi yao na kuwa wakimbizi.../