Wakimbizi wa Sudan Kusini: Askari 'wamewachinja raia kama wanyama'
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema watu zaidi ya 6,000 wamekimbia makazi yao nchini Sudan Kusini na kukimbilia wilaya ya kaskazini mwa Uganda ya Lamwo kujisalimisha na mauaji ya raia yanayofanywa na askari wa serikali ya Juba.
Taarifa iliyotolewa na UNHCR imeeleza kuwa raia wengine kutoka mji wa Pajok katika mkoa wa Equatoria nchini Sudan Kusini wamekuwa wakijificha vichakani ili kutafuta njia ya kufikia eneo la usalama nchini Uganda.
Ikiwanukuu wakimbizi hao, taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa vikosi vya jeshi la serikali ya Sudan Kusini vimekuwa vikiua raia wa mji huo kiholela.
Msemaji wa UNHCR Rocco Nuri, ametangaza kuwa wakimbizi waliokimbilia mjini Lamwo nchini Uganda wameieleza timu ya shirika hilo simulizi za kutisha za ukatili na unyanyasaji dhidi ya raia unaofanywa na wanajeshi wa serikali na kuongeza kuwa wakimbizi wengi wameshuhudia wapendwa wao wakipigwa risasi au kuchinjwa kama wanyama.
Hali hiyo imejitokeza baada ya kuzuka mapigano mjini Pajok siku ya Jumatatu iliyopita baina ya vikosi vya serikali na waasi, eneo la Sudan Kusini ambalo awali lilikuwa na amani.
"Familia zimekimbilia kila upande. Wale walioshindwa kukimbia wameripotiwa kupigwa risasi, wakiwemo wazee na watu wasiojiweza", amefafanua msemaji huyo wa UNHCR.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Uganda, hadi sasa imeshapokea wakimbizi zaidi ya 832,000 kutoka Sudan Kusini wakiwemo zaidi ya 270,000 walioko kwenye kambi ya Bidibidi, ambayo ndani ya muda wa miezi minane imebadilika kutoka ardhi tupu na kuwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani…/