Homa ya uti wa mgongo yauwa watu karibu 440 Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27504-homa_ya_uti_wa_mgongo_yauwa_watu_karibu_440_nigeria
Idadi ya watu walioaga dunia kwa kushukiwa kuugua homa ya uti wa mgongo imefikia 438, huku maafisa wa nchi hiyo wakianzisha kampeni ya kutoa chanjo ili kudhibiti mlipuko wa homa hiyo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Apr 09, 2017 02:37 UTC
  • Homa ya uti wa mgongo yauwa watu karibu 440 Nigeria

Idadi ya watu walioaga dunia kwa kushukiwa kuugua homa ya uti wa mgongo imefikia 438, huku maafisa wa nchi hiyo wakianzisha kampeni ya kutoa chanjo ili kudhibiti mlipuko wa homa hiyo.

Kitengo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria kimetoa taarifa kikieleza kuwa, kumeripotiwa wagonjwa 3959 wanaoshukiwa kuugua homa ya uti wa mgongo katika majimbo 19 kote nchini humo; huku watu 181 wakithibitishwa kuambukizwa homa hiyo.  Itafahamika kuwa mlipuko wa sasa wa homa ya uti wa mgongo ambao ni aina C ulioiathiri Nigeria, ni mlipuko ambao ni nadra kushuhudiwa. Nigeria mara kwa mara imekuwa ikiathiriwa na homa ya uti wa mgongo aina ya A. Kundi kuu lililoathirika na homa hii ni watoto walio na umri wa kuanzia miaka 5 hadi 14. Alhamisi iliyopita maafisa husika wa Nigeria walianzisha kampeni kubwa ya utoaji chanjo katika jimbo la Zamfara kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ambacho ni kitovu cha mlipuko wa ugonjwa huo. Kampeni hiyo ya chanjo inatazamia kuwafikia watu laki tano wenye umri wa kuanzia miaka 2 hadi 29.

Chanjo ya homa ya uti wa mgongo ikitolewa kwa watoto katika jimbo la Zamfara Nigeria