Askari wasiopungua watano wauawa Nigeria katika mapigano na wanamgambo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27586-askari_wasiopungua_watano_wauawa_nigeria_katika_mapigano_na_wanamgambo
Askari kadhaa wa jeshi na polisi wameuawa katika mapigano yaliyotokea baina ya vikosi hivyo vya usalama na wanamgambo wanaobeba silaha kusini magharibi mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 10, 2017 10:16 UTC
  • Askari wasiopungua watano wauawa Nigeria katika mapigano na wanamgambo

Askari kadhaa wa jeshi na polisi wameuawa katika mapigano yaliyotokea baina ya vikosi hivyo vya usalama na wanamgambo wanaobeba silaha kusini magharibi mwa Nigeria.

Shirika la habari la Nigeria NAN limemnukuu Kamishna wa Habari na Stratejia, Steve Ayorinde akitangaza kupitia taarifa kuwa askari polisi wasiopungua wanne na mwanajeshi mmoja waliuawa hapo jana muda mfupi baada ya kuokolewa watu kadhaa waliokuwa wakishikiliwa mateka kwenye maficho ya wanamgambo katika eneo la Ikorodu katika jimbo la Lagos kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Ayorinde ameongeza kuwa, kabla ya kuuawa, askari hao wa usalama walikuwa wamesha wakomboa mateka kadhaa.

Steve Ayoride, Kamishna wa habari na Stratejia

Serikali ya Abuja, mbali na kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram ambalo limevuruga usalama wa maeneo mengi ya nchi hiyo, inakabiliwa pia na uasi wa makundi ya wanamgambo wa eneo la Niger Delta kusini mwa nchi pamoja na mapigano ya kikabila.

Kutokana na kushindwa serikali ya Nigeria kulitokomeza kundi la kigaidi la Boko Haram pamoja na kutoweza pia kuzima uasi wa makundi ya wanamgambo, maelfu ya raia wameuawa hadi sasa na wengine zaidi ya milioni mbili na laki tano wamelazimika kuwa wakimbizi.../