Apr 12, 2017 07:18 UTC
  • Idadi ya watoto wanaotumiwa katika hujuma za Boko Haram yaongezeka

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umeeleza kushtushwa kwake na ongezeko la watoto wadogo kutumiwa katika hujuma za kujitolea muhanga za kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Marie-Pierre Poirier, Mkurugenzi wa UNICEF katika eneo la magharibi na katikati mwa Afrika amesema idadi ya watoto wadogo wanaotumiwa na Boko Haram katika mashambulizi ya mabomu ya kujitolea muhanga imeongezeka kwa kiasi kikubwa kinachotia wasiwasi.

Amesema mwaka 2014, ni watoto wanne tu ndio waliotumiwa katika hujuma za kigaidi za Boko Haram huku mwaka 2015 idadi hiyo ikiongezeka hadi 56. Afisa huyo wa UNICEF ameongeza kuwa, idadi hiyo ilididimia pakubwa mwaka 2016 ambapo watoto 30 walitumiwa, lakini inavyoonekana, imeanza kupanda tena mwaka huu kwa kuzingatia kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka huu 2017, watoto 27 wameshatumika katika mashambulizi hayo.

Moja ya hujuma za kujitolea muhanga za Boko Haram

Kadhalika Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umebainisha kuwa, aghalabu ya watoto wanaotumiwa katika hujuma hizo za kigaidi za Boko Haram ni wasichana ambao wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mabomu hadharani katika maeneo ya umma katika nchi za Nigeria, Chad, Niger na Cameroon.

Huku hayo yakiarifiwa, Patrick Rose, mshirikishi wa kieneo wa UNICEF amesema mamia ya watoto wanaohusishwa na Boko Haram wanazuiliwa katika mazingira magumu, bila matibabu ya kimwili na kisaikolojia na kutenganishwa na wazazi kwa vipindi virefu katika gereza la kijeshi la Giwa huko Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Hii ni licha ya serikali kuwaachia huru watoto, wanawake na wazee 600 waliokuwa wakizuiliwa katika gereza hilo Jumatatu iliyopita. 

 

Tags