Rais wa Nigeria: Tunaendelea na mazungumzo ili kuwakomboa wasichana wa Chibok
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27720-rais_wa_nigeria_tunaendelea_na_mazungumzo_ili_kuwakomboa_wasichana_wa_chibok
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema, serikali yake inaendelea na mazungumzo ili kufanikisha kuachiliwa huru idadi iliyosalia ya wasichana wa shule ya eneo la Chibok waliotekwa nyara na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 13, 2017 12:03 UTC
  • Rais wa Nigeria: Tunaendelea na mazungumzo ili kuwakomboa wasichana wa Chibok

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema, serikali yake inaendelea na mazungumzo ili kufanikisha kuachiliwa huru idadi iliyosalia ya wasichana wa shule ya eneo la Chibok waliotekwa nyara na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Buhari ameyaeleza hayo kupitia taarifa aliyotoa leo ikiwa imesalia siku moja kabla ya kuwadia kumbukumbu ya mwaka wa tatu tangu wanafunzi wa kike 276 walipotekwa nyara na kundi hilo.

"Serikali inaendelea kufanya mawasiliano mtawalia kupitia mazungumzo na kwa kutumia intelijinsia ya ndani ili kuhakikisha wasichana waliosalia na watu wengine waliotekwa nyara wanaachiwa huru bila ya kudhuriwa", ameeleza Buhari kupitia taarifa yake hiyo.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria

Ameongeza kuwa wamewasiliana na wanaowashikilia wasichana hao kupitia waunganishi wa ndani na wa kimataifa na kwamba serikali iko tayari kufanya lolote liwezekanalo kuhakikisha wasichana hao wote wanaachiwa huru.

Serikali ya Abuja imetoa ahadi mara kadhaa ya kuwakomboa wanafunzi hao wa shule ya eneo la Chibok ambapo mwezi Oktoba mwaka jana Rais Buhari mwenyewe alisema jitihada zinazofanywa zitaongezwa "maradufu". Aidha akatangaza kuwa kundi la Boko Haram liko tayari kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuwaachilia huru wasichana wengine 83 lakini hakuna mwanafunzi aliyeachiwa hadi sasa hali ambayo imezusha lawama kali za makundi mbalimbali kuhusiana na jinsi serikali yake inavyolishughulikia suala hilo.

Wasichana walioachiwa huru

Zaidi ya wasichana 20 waliachiwa huru mwezi Oktoba kupitia makubaliano yaliyosimamiwa na shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu huku wengine kadhaa wakifanikiwa kutoroka. Hata hivyo wanafunzi 195 wanaaminika kuwa wangali wako mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram

Hii ni katika hali ambayo Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia watoto UNICEF ulitangaza jana kuwa utumiaji watoto waliotekwa nyara katika mashambulio ya kujitoa mhanga yayofanywa na Boko Haram umeongezeka kwa kasi katika mwaka huu…/