Mapatano kuhusu mustakabali wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28608-mapatano_kuhusu_mustakabali_wa_libya
Hatimaye, baada ya duru kadhaa za mazungumzo, Khalifa Haftar Kamanda wa Jeshi la Kitaifa la Libya na Fayez Al Siraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Maelewano ya Kitaifa wamehitimisha hitilafu zao na kufikia mapatano kuhusu utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 04, 2017 02:19 UTC
  • Mapatano kuhusu mustakabali wa Libya

Hatimaye, baada ya duru kadhaa za mazungumzo, Khalifa Haftar Kamanda wa Jeshi la Kitaifa la Libya na Fayez Al Siraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Maelewano ya Kitaifa wamehitimisha hitilafu zao na kufikia mapatano kuhusu utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mapatano hayo,  Haftar na Siraj wataunda jeshi moja la kitaifa na pia pande mbili zimeahidi kuwa, miezi sita baada ya mapatano hayo, kutafanyika uchaguzi wa rais na bunge nchini Libya.

Kamanda wa Jeshi la Libya na Waziri Mkuu wa Serikali ya Maelewano ya Kitaifa wameafikiana kuhusu kuundwa Baraza la Urais ambalo litajumuisha kamanda wa jeshi, waziri mkuu na spika wa bunge.

Hali kadhalika wameafikiana kuhusu kupambana na ugaidi na kuyavunja makundi ya wabeba silaha.  Pande mbili pia zimekubaliana kuwa serikali haipaswi kuwa chini ya usahwishi wa makundi ya wabebe silaha huku wakisisitiza udharura wa kuheshimiwa na kutekelezwa maamuzi ya mahakama za nchi hiyo.

Mgogoro wa kisiasa Libya umekuwa ukiendelea kwa miaka kadhaa sasa. Nchi hiyo ilitumbukia katika mgogoro mkubwa mwaka 2011 baada ya kuangushwa dikteta wa muda mrefu wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.

Kushadidi mgogoro huo kulipelekea Umoja wa Mataifa kuanzisha jitihada za upatanishi mwaka 2015 kupitia mjumbe wake maalumu. Mjumbe huyo amekuwa akifanya mazungumzo na makundi ya Libya na pia nchi za eneo. Mazungumzo hayo yamekuwa yakifanyika katika mji wa  Skhirat nchini Morocco ambapo makundi mbali mbali ya kisiasa yametia saini mapatano yaliyopelekea kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. Inatazamiwa kuwa serikali hiyo itaunda  baraza la mawaziri na hivyo kuhitimisha mgogoro wa Libya na kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru nchini humo.

Ingawa serikali hii imekuwa ikijitahidi kurejesha utulivu Libya kwa miezi kadhaa sasa, lakini kutokana na ukosefu wa uungaji mkono kisheria, yaani kutopigiwa kura ya imani bungeni, serikali hiyo haijaweza kuendeleza shughuli zake ipasavyo. Baadhi ya makundi ya kisiasa ndani ya nchi hiyo yanaipinga serikali ambayo haijatokana na kura za moja kwa moja za wananchi.

Kutotambuliwa rasmi serikali ya umoja wa kitaifa ni jambo ambalo limeongeza malumbano ya kisiasa nchini humo. Libya ni kati ya nchi muhimu zaidi katika eneo la Afrika Kaskazini, na kutokana na nafasi yake ya kipekee ya kijiograifa na hifadhi kubwa ya mafuta na gesi, daima imekuwa ikikodolewa macho ya tamaa na madola ya kibeberu.

Kwa msingi huo,  kuwepo makundi mbali mbali ya wanamgambo ambayo yanataka  kupewa nafasi serikalini na kwa upande wa pili uingiliaji wa  nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ni nukta ambazo zimechangia kuendelea kutokota mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati zinatekeleza sera za kujipenyeza katika nchi za Kiafrika na hivyo kuunga mkono makundi ya wanamgambo na kwa msingi huo kuchochea moto wa mifarakano nchini humo ili ziweze kufikia maslahi yao haramu.

Wanamgmabo katika mapigano nchini Libya

Aidha kuongezeka mapigano na ukosefu wa uthabiti ni mambo ambayo yamepelekea Libya kugeuka kuwa kituo cha makundi ya kigaidi kama vile ISIS au Daesh. Kundi hilo la kitakfiri linaitazama Libya kama uwanja wa kutekelezea jinai na kituo cha kupanga njama dhidi ya nchi zingine za eneo. Pamoja na hayo, katika miezi ya hivi karibuni majeshi ya Libya yamefanikiwa kuwatimua magaidi wa ISIS kutoka miji kadhaa ya nchi hiyo na oparesheni hiyo ingali inaendelea. Katika upande wa pili kukosekana ulinzi katika mipaka ya nchi hiyo kumepelekea Libya kugeuka kuwa kitovu cha magenge hatari ya wafanya biashara haramu ya kusafirisha biadamu. Idadi kubwa ya wahajiri wanatumbukia katika mitego ya magenge hayo na hata kutumika kama watumwa huku wengine wakipigwa na dhoruba na kughiriki katika Bahari ya Mediterenea wanapojaribu kuingia barani Ulaya kinyume cha sheria.

Kwingineko hali ya ndani ya Libya pia si shwari kwani maeneo mengi ya nchi hiyo sasa yanakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi.

Matatizo hayo yote yamepelekea kushika kasi jitihada za kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuhitimisha mgogoro wa kisiasa nchini humo. Katika upande mwingine, Libya pia inadiriki kuwa inakabiliwa na hatari ya kugawanyika vipande vipande na hivyo wanasiasa hawakuwa na budi ila kufikia mapatano ambayo yanaweza kuiokoa nchi hiyo na kuiletea mwanga wa matumaini.