Viongozi wa makundi makuu Libya wakutana ili kupunguza mivutano
Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya imesema kuwa mazungumzo ya hivi karibuni baina ya Khalifa Haftar na Fayez al Sarraj ni hatua muhimu kuelekea kuleta hali ya kuaminiana na kutatua mgogoro wa miaka mingi wa nchi hiyo.
Wizara hiyo imetoa taarifa na kusema kuwa, mazungumzo baina ya Jenerali Mstaafu Khalifa Haftar, Mkuu wa Jeshi la Libya mashariki mwa nchi hiyo, na Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya yaliyofanyika nchini Imarati na hatua muhimu sana ya kuleta kuaminiana na mapatano ya kitaifa na inaweza kupelekea kupatikana utulivu wa kisiasa na kuimarishwa usalama nchini humo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya pia imewataka wananchi wa nchi hiyo kuunga mkono juhudi za kufufua umoja wa wa kitaifa na kukomesha mivurugano na migawanyiko hasimu ya kisiasa na kijamii nchini humo.
Khalifa Haftar na Fayez al Sarraj walikutana siku ya Jumanne mjini Abu Dhabi Imarati na kufikia makubaliano kuhusu utatuzi wa hitilafu za pande hizo mbili.
Viongozi hao wawili wamekubaliana pia kuunda jeshi moja na kusimamia kwa pamoja uchaguzi wa Rais na Bunge katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Libya haijawahi kushuhudia utulivu tangu wakati wa kampeni za kumpindua Kanali Muammar Gaddafi, kiongozi wa zamani wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika mwaka 2011. Nchi za Marekani, Ulaya pamoja na za eneo hilo zinalaumiwa kwa kushadidisha machafuko na ukosefu wa amani nchini humo.